Monday, November 7, 2022

UTAJIRI WENYE UCHUNGU - 4

Sehemu Ya Nne (4)



*****


Dylan hakuamini kama mke wake alikuwa amejifungua watoto mapacha, pale nje alipokuwa alikuwa akirukaruka kwa furaha huku akimkumbatia kila mtu aliyepita mbele yake.


Alibaki mahali hapo kwa dakika zaidi ya arobaini na ndipo baadaye mkewe alipotolewa na kupelekwa katika chumba cha mapumziko ambapo huko kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa na watoto wao.


Hakutaka mke wake awe huko, alikuwa bilionea mkubwa hivyo alichokitaka ni mke wake kupelekwa katika chumba kingine cha peke yake, na hicho ndicho kilichofanyika haraka sana.


Dylan alibaki akimwangalia mkewe, alionekana kuwa na furaha muda wote, hakuamini kama kweli leo hii alikuwa akiitwa baba. Alichukua simu yake na kumpigia baba yake na kumpa taarifa hizo, baba yake alifurahi kwa kupata wajukuu.


Hakuishia hapo tu bali alichokifanya ni kuwapigia marafiki zake wengine akiwemo Catherine na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea, msichana huyo hakutaka kubaki nyumbani, japokuwa ilikuwa ni usiku wa manane, akaamka na kuelekea hospitalini.


“Wa kiume ataitwa Patrick, na wa kike ataitwa Patricia,” alisema Dylan huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.


Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumshukuru mke wake kwa zawadi nzuri aliyompa ambayo hakuweza kuifikiria kabla. Kila alipomwangalia, kwa furaha aliyokuwa nayo, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.


“Nashukuru sana mke wangu,” alisema Dylan huku akimwangalia Katty usoni.


“Asante kwa kushukuru...nililia sana kwa ajili ya hawa watoto,” alisema Katty.


Wala haikuchukua muda mwingi, Catherine akaingia ndani ya chumba hicho, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwafuata watoto wale, akawaangalia, moyo wake ukaridhika, furaha ya ajabu ikampata moyoni mwake.


Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa furaha ya familia hiyo. Dylan akajipa likizo ya mwezi mzima, hakutaka kutoka ndani ya nyumba yake, alibaki huko huku muda wote akiwa pembeni ya watoto wake.


Japokuwa usiku walikuwa wakilia sana, hakujali, kelele zao zilikuwa ni furaha tele kwake. Yeye ndiye aliyekuwa na jukumu la kuwabadilisha nguo, yeye ndiye alikuwa na jukumu la kuzifua nguo zao kwani hakutaka kabisa wafanyakazi wafanye kitu chochote kwa ajili ya watoto wake.


Mwezi ulipokatika, hapo ndipo alipoanza kwenda kazini. Huko, hakuwa mkaaji sana, ilikuwa ni lazima arudi nyumbani mapema mno. Kila mtu aliyekuwa akimtazama, alionekana dhahiri kuwa na furaha kubwa moyoni mwake, alimsalimia kila mtu na kila aliporudi nyumbani, ilikuwa ni lazima awe na mfuko uliojaa nguo kwa ajili ya watoto wake.


“Nitahakikisha nawapa kila kitu,” alimwambia mke wake.


“Kweli?”


“Ndiyo! Nimekuwa na furaha mno, maisha yangu yamebadilika, wameniletea kitu moyoni mwangu ambacho sikuwa nikikifikiria kabla,” alisema Dylan huku akiwa na Patricia mikononi mwake.


Siku ziliendelea kukatika, miezi ikaenda mbele mpaka mwaka ulipokatika, bado biashara yake ilikwenda vizuri, mafanikio yaliendelea kumiminika. Mwaka wa pili ukaingia, wa tatu mpaka wa nne ambapo mapacha hao wakaanza kusoma chekechea.


Jukumu la kuwapeleka shuleni lilikuwa lake, hakutaka mtu yeyote achukue jukumu hilo. Watoto hao walikuwa wazuri wa sura, walifanana mno. Patricia ambaye ndiye alikuwa Kulwa, sura yake iliwachanganya watu wengi, urembo wake uliwafanya watu kuona kwamba mtoto huyo angekuwa msichana mrembo mno siku za usoni.


Shule waliyokuwa wakisoma ilikuwa ni St. Pius International School, hiyo ilikuwa miongoni mwa shule za matajiri, watoto waliokuwa wakisoma shuleni hapo, wazazi wao walikuwa matajiri au viongozi wa serikali kama mawaziri.


Mbali na utajiri, pia serikali iliwasomesha watoto waliokuwa na uwezo kiakili shuleni hapo. Ilikuwa ni shule ya vipaji lakini upande wa pili ilikuwa ni shule ya matajiri.


Kila siku ilikuwa ni lazima kwa Dylan kuwapeleka shule watoto wake na kuwarudisha nyumbani. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, hakutaka kuona wakipata tabu yoyote ile, kwake, watoto wake ndiyo walikuwa kila kitu.


Miaka haikumsubirii mtu yeyote ile, baada ya kufikisha miaka nane, uzuri wa Patricia ukazidi kuongezeka, vijana wengi shuleni hapo wakamtolea macho, japokuwa alionekana kuwa mtoto lakini umbo lake lilikuwa kubwa, vijana wengi wakaanza kuweka mazoea na kijana wa kwanza kabisa kuwa karibu naye aliitwa Tenny Andrew.


Huyu alikuwa mtoto wa waziri mstaafu nchini Marekani, Bwana Carthbert Andrew. Alikuwa miongoni mwa watoto waliokuwa na akili nyingi shuleni hapo. Kila mmoja alitamani kuwa karibu na kijana huyo ambaye kama ingekuwa Tanzania, basi tungesema kwamba kijana huyo alikuwa darasa la saba huku Patricia akiwa darasa la tano.


Ukaribu wao ulianza taratibu, watu wengi wakaanza kuhisi kwamba nyuma ya pazia kulikuwa na kitu kinaendelea. Walimu hawakutaka kukaa kimya, walichokifanya ni kumuita Tenny na kuzungumza naye, walimwambia kabisa kwamba ukaribu wake na msichana Patricia uliwatia shaka lakini yeye mwenyewe hakutaka kukubaliana nao.


“There is nothing is going on, trust me,” (hakuna kinachoendelea, niamini) alisema Tenny.


Huku nyumbani, Bwana Dylan hakutaka kuvuruga ratiba yake. Kila siku ilikuwa ni lazima kuwapeleka watoto wake shuleni na kisha kuwarudisha kila ilipofika mchana.


Siku ziliendelea kukatika mpaka pale ambapo Bwana Dylan alipotaka kuwafanyia sapraizi watoto wake kwa ajili ya siku yao ya kuzaliwa.


Siku hiyo hakutaka kuwapeleka shuleni, alipotoka ofisini mapema sana, akapitia supamaketi ambapo akawanunulia keki kubwa, zawadi nyingine na kisha kurudi nyumbani.


Alipofika huko, akamuita mke wake na kumwambia kile alichotaka kukifanya. Kilionekana kuwa kitu kizuri sana. Ili kitu kile kikamilike, ilikuwa ni lazima dereva ndiye awafuate shuleni huko siku hiyo.


Akawasiliana na dereva na hivyo kwenda kuwachukua. Yeye na mkewe walibaki nyumbani, waliandaa mazingira mazuri, wakawaita watu wengine kwa ajili ya kusherehekea nao.


Muda ukaanza kwenda, ulikwenda na kwenda, kitu ambacho kiliwashangaza na kuwashtua ni kwamba watoto hao hawakufika nyumbani. Haikuwa kawaida, shule haikuwa mbali na nyumbani hapo, wakampigia simu dereva ili kumuuliza walikuwa wapi na kitu gani kilikuwa kikiendele, kilichowatisha, simu ya dereva huyo haikuwa ikipatikana.


“I can’t reach him on the phone,” (Simpati kwenye simu) alisema Bwana Dylan.


“What?” (Nini?) aliuliza mkewe.


“I can’t reach him,” (Simpati)


Kila mmoja alichanganyikiwa, kile walichokisikia hakikuaminika kabisa, walichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo, seherehe ile iliyoandaliwa, ikavurugika kwa muda. Bwana Dylan akaingia ndani ya gari, aliendesha gari yeye mwenyewe na tena kwa kasi kubwa.


Wakafika shuleni, hakukuwa na mwanafunzi yeyote yule, wakaelekea mpaka katika ofisi ya walimu na kuwauliza kama dereva alifika shuleni hapo. Wakaambiwa kwamba alifika, aliwachukua watoto hao na kuondoka nao.


“Kwani nyumbani hawakufika?” aliuliza mwalimu mmoja.


“Hawakufika! Aliwachukua muda gani?”


“Kama saa moja lililopita!”


“Watakuwa wapi?”


“Hata sisi tunashangaa...”


Kweli walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea, walichokifanya ni kujaribu tena kumpigia simu dereva, kama kawaida majibu yalikuwa yaleyale, simu haikupatikana. Walichanganyikiwa, dakika ziliendelea kusonga mbele, waliogopa hivyo walichokifanya ni kuwasiliana na polisi.


“Hatujui walipo...”


Hivyo ndivyo walivyosema, polisi wakaanza kuwatafuta. Waliwatafuta kwa kuanzia kamera zao za barabarani, hawakupatikana. Walichanganyikiwa, hawakujua watoto hao walipelekwa wapi na dereva huyo.


Muda wote Katty alikuwa akilia tu, hakuwa akiamini kilichokuwa kikiendelea, Dylan, japokuwa yeye mwenyewe alikuwa na uchungu lakini hakutaka kuuonyesha waziwazi, hivyo akajitahidi kumliwaza mke wake. Mpaka inafika saa mbili usiku, polisi hawakumpata dereva wala watoto. Wakazidi kuchanganyikiwa.




Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Mike akachukua simu yake na kuanza kumpigia msichana Aisha, alitaka kuzungumza naye na kujua wakati huo alikuwa mahali gani.


Ndiyo kwanza msichana huyo alikuwa nyumbani kwake, hakuwa ametoka, alikuwa akijiandaa kwa ajili ya kupanda ndege na kwenda huko Dubai kuonana na mwanaume huyo aliyekuwa na uchu naye.


Mike akawa kwenye presha kubwa, japokuwa alikuwa chumbani hotelini lakini mara kwa mara alikuwa akikiangalia chumba hicho na kuangalia sehemu ambayo haikuwa imepangwa vizuri na kuipanga. Alikuwa na hamu ya kukutana na msichana huyo ambaye kwake alionekana kuwa mwanamke wa ndoto.


Ilipofika saa tano asubuhi, Aisha akampigia simu na kumwambia kwamba tayari alikuwa uwanja wa ndege hivyo amfuate kitu ambacho Mike alifanya haraka sana kwa kutumia magari maalumu ya kukodi yaliyokuwa hotelini hapo.


Alipofika, huku kofia ikiwa kichwani mwake, akateremka na kuanza kuelekea sehemu ya mapokezi, japokuwa alikuwa mtu maarufu kidogo kutokana na utajiri aliokuwa nao lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyemgundua, hata Aisha alipotoka, naye alijificha kwa kuvaa baibui, hijabu na nikabu.


Msichana huyo alimuona Mike japokuwa mwanaume huyo hakuwa amemgundua Aisha. Msichana huyo akamsogelea Mike na kusimama mbele yake, kitendo cha Mike kuyaona macho ya Aisha tu, akajua ndiye mwenyewe, hakuzungumza kitu, akampokea, akarudi garini na kuanza kuelekea hotelini.


“Nimekukumbuka sana mpenzi,” Mike alimwambia Aisha huku akiachia tabasamu pana na macho yake mara mojamoja yakiangalia mbele.


“Umekumbuka nini kutoka kwangu?” aliuliza Aisha huku naye akirudisha tabasamu pana.


“Kila kitu! Hayo macho yako, huwa yananiacha hoi sana,” alisema Mike huku akimwangalia vizuri msichana huyo.


Kadiri alivyomwangalia, moyo wake ulizidi kumpenda msichana huyo, alikuwa mzuri wa sura, kila alipoongea, sauti yake ilikuwa ikimtetemesha moyoni mwake. Humo ndani ya gari, Aisha akapata muda wa kubadilisha mavazi, akavua baibui lake na kupigilia suruali ya jinsi, ila kichwani hakuacha hijabu na miwani mikubwa ya kike.


Walichukua dakika kadhaa, wakafika katika hoteli hiyo ambapo wakateremka na kuingia ndani. Hakukuwa na watu waliowagundua, walikwenda kwenye lifti ambayo iliwapeleka mpaka katika floo ambayo Mike ndiyo aliyochukulia chumba.


“Karibu sana,” alisema Mike mara baada ya kuingia ndani.


“Asante sana, hivi ni kwa ajili yangu?”


“Ndiyo! Nimeandaa kwa ajili yako tu mrembo,” alisema Mike.


Mbele yao kulikuwa na meza iliyokuwa na vyakula kadhaa huku maua yakiwa pembeni. Aisha akabaki akiiangalia meza ile, moyo wake ulishtuka, hakuamini kuona kile alichokiona. Akakisogelea na kuangalia vizuri, moyo wake ukampenda Mike zaidi na zaidi.


Wakaelekea mezani na kuanza kunywa juisi, muda wote huo walikuwa wakiangaliana kimahaba tu. Kila mmoja alivutiwa na mwenzake, walipendana kiasi kwamba mbele yao hakukuwa na kitu kilichokuwa kikionekana zaidi ya ndoa tu.


Walinyweshana na kuonyeshana mapenzi ya njiwa. Baada ya kumaliza kunywa juisi, hakukuwa na kingine kilichoendelea zaidi ya kupanda kitandani na kuanza kushikana hapa na pale.


Aisha alikuwa akitetemeka kwa woga, hakuwahi kuwa kitandani na mwanaume, ni kweli alikuwa na miaka ishirini na nne lakini bado hakuwahi kumpa nafasi mwanaume yeyote yule kutokana na sheria kali iliyokuwepo nchini mwao.


“Mbona unatetemeka hivyo?” aliuliza Mike huku akiachia tabasamu pana.


“Sijawahi!”


“Kweli?”

“Ndiyo!”


“Hata siku moja?”


“Ndiyo! Sijawahi kabisaaa....” alijibu Aisha.


Mike akaachia tabasamu pana, hakuamini kusikia kwamba Aisha alikuwa msichana mbichi kabisa. Hakutaka kuchelewa, alijua namna ya kuwatuliza wanawake wa namna hiyo kitandani. Akafanya maandalizi yote, alipofanikiwa, mchezo ukaanza.


Muda wote Aisha alikuwa mtu wa kulalamika tu, alilia kwa kuwa alisikia maumivu makali chini ya kitovu. Muda mwingi alikuwa akimsukuma Mike atoke juu yake lakini mwanaume huyo alionekana kuwa mbishi, hakutaka kutoka wala kusogea popote pale.


Mchezo huo ulichukua dakika arobaini na tano, kila mmoja alikuwa hoi. Aisha hakuamini kama mwisho wa siku alilala na mwanaume kitandani. Kwake ilikuwa ni kama kuivunja ahadi aliyowaambia wazazi wake kwamba kamwe mwanaume wa kwanza kulala naye angekuwa mume wake, tena kipindi ambacho wapo ndoani kabisa.


“Mike, nimefanya nini tena?” aliuliza Aisha huku akianza kububujikwa na machozi.


“Kufanya nini tena?”

“Sikutaka kufanya hivi! Sikutaka Mike...” alisema Aisha huku akivuta shuka na kuanza kulia.


“Najua...najua Aisha, acha kulia mpenzi...”


“Mike, ninajuta, kwa nini nimefanya hivi? Nitauficha wapi uso wangu mimi?” aliuliza Aisha huku akilia kitandani pale. Kila alipomwangalia Mike, moyo wake ulimuuma mno.


“Kwani kuna tatizo gani?”


“Mike! Sikutaka kufanya hili kabla ya ndoa, niliuandaa usichana wangu kwa ajili ya mume wangu tu, kwa nini nimefanya na wewe kabla ya ndoa?” aliuliza msichana huyo, kulia hakuacha, muda wote machozi yalikuwa yakimtoka tu.


“Aisha...usilie mpenzi, nakuahidi kwamba nitakuoa!”


“Unanidanganya Mike!”


“Niamini! Ninakupenda sana, sitokuacha, nitakuoa, utakuwa mke wangu,” alisema Mike kisha kumkumbatia msichana huyo ambaye machozi yake yakatiririka mashavuni na kumwagika mgongoni mwa Mike.


Aisha hakukaa sana Dubai, siku iliyofuata tu, akaondoka na kurudi Kuwait. Moyo wake ulikuwa na maumivu kutolewa usichana wake na mwanaume huyo lakini wakati mwingine alikuwa akijifariji kwa kuhisi kwamba mwanaume huyo ndiye angekuja na kuwa mume wake wa ndoa.


Hawakuacha kuwasiliana, muda mwingi walikuwa wakiongea kwenye simu, walipendana, bado Mike aliendelea kumwambia Aisha kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumuoa na kuwa mke wake wa ndoa.


“Na vipi kuhusu dini?” aliuliza Aisha.


“Sijajua, ila nitakuoa tu.”

“Kweli?”

“Niamini!”


Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki mbili kupita, Aisha akaanza kujisikia tofauti mwilini mwake, akaanza kutapika hali iliyomfanya kukosa raha kabisa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mwilini mwake, alichokifanya ni kumpigia simu Mike ambaye alikuwa nchini Marekani na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea.


Mike alivyoambiwa hivyo tu, akajua kwamba msichana huyo alikuwa mjauzito. Hakutaka kumficha, alimwambia aende akapime mimba kitu ambacho Aisha alipingana nacho.


“Haiwezi kuwa mimba!”


“Usiseme hivyo Aisha...nenda...”


“Sawa!”


Japokuwa hakuwa akiamini lakini akafanya hivyo ili kumfurahisha mpenzi wake tu. Akaenda mpaka katika Hospitali ya Al Tawfiq iliyokuwa katikati ya Jiji la Al Asimah kwa ajili ya kupima mimba.


Alipofika huko, moja kwa moja akaenda kwa daktari ambaye alimpima kipimo alichokitaka, kitu ambacho hakuamini hata mara moja ni pale alipopewa majibu kwamba alikuwa na mimba ya wiki mbili.


“Unasemaje?” aliuliza huku akionekana kutokuamini.


“Una mimba ya wiki mbili!” alijibu daktari. Aisha akachanganyikiwa kwani kupata mimba kabla ya ndoa, adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe hadharani mpaka kufa pasipo kujali kama alikuwa binti wa mfalme au la.


****


Aisha alichanganyikiwa, hakuamini kile alichoambiwa, alimwangalia daktari yule mara mbilimbili na kumuuliza kama vipimo vyake vilionyesha sahihi, daktari huyo akamwambia kwamba vilikuwa sahihi na hata aliporudia, vilionyesha vilevile kwamba alikuwa mjauzito.


Akakosa furaha, akabaki akilia, hakuamini kile kilichotokea, aliifahamu nchi yao, sheria kali za dini hazikukutaka ufanye ujinga wowote ule, usipate mimba vinginevyo adhabu yako ingekuwa kupigwa mawe hadharani mpaka kufa.


Aisha hakutaka kubaki hospitalini hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea nyumbani kwao. Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kilichokuwa kimetokea. Alipofika nyumbani kwake, kitu cha kwanza kabisa kiliikuwa ni kujifungia chumbani na kuanza kulia.


Moyo wake ukamuuma, akajiona akiwa amefanya kosa kubwa sana maisha mwake. Hakutaka kabisa kubeba mimba akiwa na umri huo, kitendo cha kushika mimba tayari kilimaanisha kwamba kilichofuata mbele ni kifo tu.


“Mpenzi...” aliita Aisha huku akilia kwenye simu.


“Niambie mpenzi...”


“Nina mimba...”


“Kweli?”

“Ndiyo!”


“Hureee...” alisikika Mike akishangilia.


Kwa Aisha, hakukuwa na muda wa kushangilia zaidi ya kuwa na maumivu makali moyoni mwake. Mike alitakiwa kuwa na furaha hivyo kwani inawezekana alitafuta sana mtoto au alitamani kuzaa na mwanamke mrembo kama alivyokuwa.


Kwa msichana Aisha, furaha ya Mike ilikuwa ni sawa na kuukandamiza msumali wa moto moyoni mwake kwani alizidi kuumia mno. Siku hiyo hakutoka ndani ya chumba chake, alibaki humohumo, akizungumza na Mike na kumwambia hatari iliyokuwa mbele yake.


“Kwa hiyo wakijua watakuua?” aliuliza Mike.


“Ndiyo! Wataniua mpenzi...”


“Hapana! Hawawezi kumuua mwanamke mwenye mtoto wangu...” alisema Mike huku akionekana kushtuka.


Wakati wakizungumza kwa simu, tayari ilikuwa ni saa saba mchana hapo Kuwait. Hata kabla simu haijakata, mara Aisha akasikia mlango ukigongwa, akasimama na kuufuata, alipoufungua tu, polisi wawili walisimama mbele yake huku wakiwa na daktari.


“Upo chini ya ulinzi...” alisema polisi mmoja.


“Nimefanya nini?”

“Umeisaliti dini yetu...”


“Kivipi?”

“Umepata mimba! Uongo?” aliuliza polisi huyo huku mwenzake na daktari wakimwangalia Aisha.


Lengo la kufika na daktari huyo ilikuwa ni kumchukua vipimo Aisha pale ambapo angekataa kwamba hakuwa na mimba. Aisha alinyog’onyea mwili, hakuamini kabisa kile alichokisikia kutoka kwa madaktari hao, swali kubwa ambalo lilimjia kichwani mwake, watu hao walijuaje kama alikuwa na mimba?


Polisi hawakutaka kuchelewa, walichokifanya ni kumfunga pingu na kuondoka naye. Njiani, Aisha alikuwa akilia sana, hakuuamini kama mwisho wa maisha yake ungekuwa namna hiyo. Akaingizwa kwenye gari na safari ya kuelekea katika Kituo cha Polisi kuanza mara moja.


***


Mara baada ya Aisha kuondoka katika Hospitali ya Al Tawfiq, moja kwa moja daktari aliyempima, Dk. Fawdhil akawasiliana na Wazee wa Baraza la Sheria la nchini Kuwait na kuwaambia kile kilichotokea.


Japokuwa kilitakiwa kuwa siri baina yake na mgonjwa hasa katika mambo yanayohusu vipimo lakini daktari huyo hakutaka kunyamaza, akachukua simu yake na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.


Wazee hao wa Baraza la Sheria hawakutaka kuchukulia jambo hilo harakaharaka, walitakiwa kuwa na ushahidi mkubwa hivyo kuwaagiza watu waende katika hospitali hiyo na kuonana na daktari huyo.


Alichokifanya ni kuwapa kuwapa majibu ya vipimo vile ambavyo wakavichukua na kuviangalia, hawakuamini baada ya kugundua kwamba msichana aliyepata mimba alikuwa binti wa mfalme wa nchi hiyo.


“?????????????????,” (msichana aliyepata mimba ni binti wa mfalme) alisema mmoja wa vijana waliotumwa waende huko.


“?????????,” (Unasemaje?)


“????????????????????,” (Ndiyo hivyo! Ni Aisha) alijibu kijana huyo.


Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama msichana huyo angeweza kufanya kitu kama hicho na wakti alijua dhahiri jinsi sheria za nchi za Uarabuni zilivyosema. Hawakutaka kubaki hospitalini hapo, walichokifanya ni kuondoka na kurudi kwa Wazee wa Baraza la Sheria ambapo wakawaambia kila kitu kilichotokea.


“Yaani unamaanisha huyuhuyu Aisha binti mfalme?” aliuliza mzee mmoja.


“Ndiyo!”

“Hapana! Siwezi kuamini!”


“Ndiyo hivyo mkuu! Ni Aisha huyohuyo!”


Walichokifanya ni kuwasiliana na waziri mkuu na kumwambia kile kilichotokea, kila mmoja aliyepata taarifa hiyo alishangaa, iweje binti wa mfalme apate mimba na wakati alizijua sheria zote kwamba msichana yeyote hakutakiwa kuzini mpaka pale atakapoolewa.

Waziri Mkuu akafanya mipango ya kuwasiliana na Mfalme Sabah Al Ahmad ambaye ndiye alikuwa baba yake Aisha. Mfalme alivyoambiwa kuhusu binti yake, hakuamini hata kidogo, alimfahamu msichana huyo, alikuwa radhi kuulinda usichana wake kwa nguvu zote lakini si kufanya uzinzi hata kabla ya kuolewa.


“Binti yangu hawezi kufanya hivi,” alisema mfalme huku akionekana kuchanganyikiwa.


“Amefanya, na vipimo hivi hapa,” alisema mzee mmoja huku akimpa karatasi iliyokuwa na majibu ya vipimo alivyochukua.


Kilichofuata baada ya kuyaangalia majibu yale ni machozi kuanza kumbubujika mashavuni mwake. Mbele yake alihisi aibu kubwa ikimkumba, aliwaona watu wote wakimsogelea na kisha kuanza kumzomea.


Kama alizishika sheria zote tena huku akiwaambia watu wengine wazishike, ilikuwaje akashindwa kumwambia binti yake? Alichanganyikiwa lakini hakuwa na jinsi, kama zilivyokuwa sheria nyingine kwamba ni msumeno, basi naye Aisha alitakiwa kukamatwa na kuhukumiwa kifo cha kupigwa risasi au mawe hadharani.


Yeye ndiye alikuwa mfalme, kwenye muda wa kuweka saini katika karatasi ya kuruhusu msichana huyo akamatwe, akaingia kwanza chumbani kwake, yeye na mkewe wakalia sana, alipotoka, hakuwa na jinsi, akasaini karatasi hiyo, Aisha alitakiwa kukamatwa, kusomewa kesi yake kisha kuhukumiwa.





Watu wengi walishangaa, hawakuamini kile walichokisikia kwamba binti wa mfalme, Aisha alikuwa amefanya mapenzi na mwanaume na kupata ujauzito. Taarifa ile ilisambaa kwa kasi kama moto wa kifuu na hata magazeti ambayo yalitoka siku hiyo yalikuwa na habari hiyo huku picha ya msichana Aisha akiwa na pingu ikionekana vizuri kabisa.


Macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa akilia kila wakati, kila alipohojiwa, hakusita kumuomba msamaha kila mmoja kwamba kile kilichotokea hakikuwa lengo lake, alifanya hivyo kwa kuwa alimpenda mwanaume huyo ambaye hakutaka kumtaja.


Selo alipolala, kila wakati alikuwa na huzuni tele, hakujua ni kwa namna gani angeweza kukiepuka kifo kilichokuwa mbele yake. Wakati mwingine alijiona kuwa mkosefu mkubwa kwa kulikosea taifa hilo, ila pamoja na yote hayo, hakumlaumu Mike, alikuwa mwanaume aliyempenda sana katika maisha yake.


Huko hakupata nafasi ya kuwasiliana na Mike, hakukuwa na simu, alikuwa kwenye ulinzi mzito ambao hata kumuona tu ilikuwa kazi kubwa. Mfalme Sabah alikuwa kwenye huzuni kubwa, kilichotokea, hakuamini, alijidharau kwa kuona kushindwa kumlinda mtoto wake asipate mimba.


Uhuru aliokuwa amempa, leo hii ndiyo ulimfanya kuwa katika hali hiyo, alijifungia chumbani na mkewe na kuendelea kulia. Ile ilikuwa sheria, hakuweza hata kuipindisha kwani kulikuwa na watu wengi huko nyuma ambao nao walipigwa mawe na risasi hadharani kwa kubambwa wakizini au hata kupata mimba.


Shirika la Haki za Binadamu Duniani (Human Rights) likaingilia kati, kile kilichotaka kutokea nchini Kuwait, hawakukubaliana nacho hata kidogo, ilikuwa ni lazima wawasiliane na serikali ya nchi hiyo na kuzungumza nayo ili isifanye kile kilichotakiwa kufanya, cha ajabu, serikali ikakataa katakata.


“Haiwezekani, hii ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya kidini, kitu hicho hatuwezi kukifumbia macho, ni lazima hukumu itolewe,” alisema msemaji wa serikali ya Kuwait.


“Lakini ni kinyume na haki za binadamu...”


“Hiyo ni huko kwenu, ila huku kwetu, kila kitu kipo kwenye misingi ya dini,” alijibu, hakuiacha simu hewani, akaikata.


Huko alipokuwa, Aisha hakutakiwa kuonana na ndugu zake, alitakiwa kukaa hukohuko, kama kuwaona angewaona siku ambayo angepelekwa mahakamani tu, tena kuwaona na si kuzungumza nao.

Siku zikaendelea kukatika, mwili wake ukakonda, ukakosa nguvu, kila siku ilikuwa ni huzuni kwake, hakuamini kama kuna siku angeweza kupata furaha maishani mwake.


Baada ya siku kadhaa, akatakiwa kufikishwa mahakamani, huko hakukuwa na muda wa kusikiliza kesi, kilichotakiwa ni kutolewa kwa hukumu juu ya kile alichokuwa amekifanya.


“??????????????????????????????? ,” (Unahukumiwa kupigwa mawe hadharani mpaka kufa) alisema hakimu, hakukuwa na kilichoendelea zaidi ya kufunga keso hiyo kwa kuwaambia watu kuwa hukumu hiyo ingefanyika wiki moja baadaye, mbele ya macho ya watu wote ili iwe fundisho.


Mahakamani hapo, ndugu zake wote walikuwepo, hukumu ilipotolewa, sauti za kilio zilisikika kutoka kwa ndugu zake, mfalme, mama yake na watu wengine. Hakuruhusiwa kuzungumza nao, akachukuliwa na kurudishwa tena sero ambapo huko akabaki peke yake akisubiri siku ya hukumu.


Dunia haikunyamaza, kila siku wanaharakati wa haki za binadamu wakahangaika ili kumnasua Aisha kwenye hukumu hiyo lakini halikuwezekana, walichanganyikiwa, hawakutaka kumuona msichana huyo mrembo aliyekuwa na mimba akihukumiwa adhabu kubwa kama hiyo.

Walijitahidi kwa kushirikiana na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi lakini juhudi zao zote hizo ziligonga mwamba, hawakuchoka, waliendelea kufanya jitihada nyingine lakini bado Waarabu walimng’ang’ania Aisha, hivyo wakaachana naye.


Humo sero, siku zilikatika kwa haraka sana, Aisha alilia mno, hakuamini kama kweli alibakisha siku chache kabla ya kifo chake. Zilipobaki siku mbili kabla ya tukio, mahakama ikalegeza msimamo kwa kuwaruhusu ndugu zake kuzungumza naye akiwa humo sero.


“Ninakufa mama...” alisema Aisha huku akilia.


“Mwanangu, mwa nini umefanya hivi?” aliuliza mama yake, naye alikuwa akilia tu.


“Mama! Nilimpenda mpenzi wangu! Najua nimekosa lakini sikuwa na jinsi, sikuwa na jinsi mama, naombeni mnisamehe,” alisema Aisha huku akilia mno.


“Aisha binti yangu! Kama ningekuwa na uwezo, ningepindisha sheria ili uachiwe huru, nimejaribu sana lakini nimeshindwa,” alisema baba yake, mfalme Sabah.


Walizungumza mengi lakini katika yote hayo, Aisha hakutaka kumtaja mtu aliyempa mimba. Hilo lilibaki kuwa swali kubwa lililomuumiza kila mtu, walitaka wamfahamu mwanaume huyo ili kama ikiwezekana naye apokee adhabu lakini Aisha hakutaka kulitaja jina lake.

Siku hizo mbili zilipokatika, mlango wa sero ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia ndani. Akamchukua Aisha, akamfunga kitambaa usoni na kuanza kutoka naye ndani ya chumba cha sero hiyo.


Walipofika nje, wakaingia ndani ya gari lililokuwa na polisi wengi kisha kuanza safari ya kuelekea katika uwanja maalumu wa kuhukumia watu, uwanja ambayo ulionekana kuwa kama laana, hata jina lake uliitwa kwa Kiarabu, Laenatan (????) yaani, Laana.


Watu walikuwa wengi njiani, wengi walitaka kuona binti huyo mrembo, Aisha, binti mfalme akichukuliwa na kwenda kupigwa mawe. Kila mahali gari hilo lilipopita, watu walimzomea Aisha, alimtia aibu baba yake, hakutakiwa kuishi tena, kitu ambacho kila mtu alitamani kukiona ni binti huyo akipigwa mawe hadharani na kufa.


Mpaka gari linafika katika uwanja huo, Aisha alikuwa amelia vya kutosha, hakukuwa na msaada wowote ule alioupata, hakuona kitu kutokana na kitambaa alichokuwa amefungwa, akateremshwa kutoka garini, akapelekwa katika sehemu uliokuwa na shimo, alitakiwa kuingizwa humo, kufukiwa na kichwa tu ndicho kibaki na hicho ndicho ambacho watu walitakiwa kukipiga mawe mpaka kufa.


Akaingizwa kwenye shimo lile, likafukiwa. Toroli lililokuwa limebeba mawe makubwa likaletwa mahali hapo, mawe yale yakateremshwa. Katika uwanja huo kulikuwa na watu zaidi ya mia tano, wale waliotaka kumpiga Aisha wakayafuata mawe tayari kwa kuanzia kutoa hukumu hiyo.


Aisha ambaye ni kichwa chake tu ndicho kilichokuwa kimebaki juu, alikuwa akilia tu, hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Alitamani kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo kuwa ndoto, ila hicho hakikuwezekana, kilichokuwa kikitokea, kilitokea kwenye maisha halisi.


“Moja, mbili...ta...” alisema mwanaume aliyekuwa akihesabu, watu wengine wakayaandaa mawe yao.

Wakati mwanaume huyo akimalizia kuhesabu, ghafla mabomu ya gesi yakaanza kupigwa mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyejua nini kilitokea, mabomu kadhaa yalipigwa mfululizo, watu wakaanza kukimbia, hakukuwa na aliyemuona mwenzake, kila kona, kulikuwa na moshi mkubwa na kuwafanya watu kukohoakohoa tu.


Aisha mwenyewe hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimeendelea, alisali sala yake ya mwisho na kitu pekee ambacho alisubiri mahali hapo ni kufa tu. Mabomu ya gesi yaliyokuwa yamepigwa yalimshtua na hakujua kitu gani kilikuwa kimetokea.


Watu walikohoa, wengine walijigonga na wenzao, uwanja huo ulibadilika, na si hapo tu hata nje ya uwanja kote huko kulipigwa mabomu hayo. Wakati Aisha akijiuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea, ghafla mbele yake akatokea mwanaume mmoja, alikuwa akitembea huku mkoni mwake akiwa na bunduki kubwa, alipomfikia, akaanza kufukua kwa kasi ya ajabu.


“We have to go,” (Tunapaswa kuondoka) alisema mwanaume huyo huku akiendelea kumfukua.


“Please don’t kill me,” (Usiniue tafadhali) alisema Aisha.


“I am not here to kill you, but to save you,” (Sipo hapa kukuua bali kukuokoa) alisema mwanaume huyo huku akiendelea kumtoa Aisha katika shimo lile.


Bado mabomu ya gesi yaliendelea kusikika kila kona hali iliyoonyesha kwamba mwanaume huyo hakuwa peke yake mahali hapo, alikuwa na wenzake ambao walikuwa wakiendelea kuyapiga mabomu hayo mahali hapo kuwatawanyisha watu zaidi.


Kwa sababu Aisha alikuwa amekaa kwenye gesi hiyo kwa kipindi kirefu, mwanaume yule akachukua kinyago kile alichokivaa na kisha kumvisha msichana huyo na kumtoa katika shimo lile.


Kilichofuatia ni kuanza kuondoka mahali hapo kuelekea sehemu iliyokuwa na gari. Moshi wa gesi ulitapakaa kila kona, ilikuwa ni vigumu mno kuona hata hatua tatu mbele lakini mwanaume yule alikuwa makini na walifanikiwa kufika mpaka kwenye gari wakiwa salama kabisa.


Walipoingia tu, na wenzake wakaja na kuingia, kilichofuatia, gari likawashwa na kuondoka mahali hapo huku Aisha akiwa na maswali mengi kichwani mwake, watu hao walikuwa ni wakina nani? Kila alipojiuliza, alikosa jibu.


Watu waliokuwa wamesogea baada ya kuona moshi wa gesi umepungua, wakasogea kule uwanjani, wakaokota mawe tayari kwa kumshambulia Aisha kama walivyotaka kufanya.


Kitu kilichowashtua, Aisha hakuwepo. Shimo lilikuwa wazi, lilifukuliwa na msichana huyo hakuwemo humo. Kila mmoja alishangaa, wakaanza kujiuliza kama msichana huyo alilifukua shimo hilo yeye mwenyewe na kukimbia au kulikuwa na mtu mwingine aliyelifukua, kila walilojiuliza, wakakosa jibu, kitu pekee walichokisema ni kwamba msichana huyo aanze kutafutwa kila kona.





Mike alishindwa kuamini kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni kwamba mpenzi wake, msichana aliyekuwa akimpenda kuliko msichana yeyote katika dunia hii alitarajiwa kuhukumiwa kwa kupigwa mawe hadharani au kupigwa risasi.


Moyo wake ulimuuma mno, hakutaka kuona msichana huyo akiuawa, alimpenda na kubwa zaidi alikipenda kiumbe kilichokuwa tumboni, alichokitaka ni baada ya miezi tisa tu.


Alijiona kuwa na kitu cha kufanya, kumuacha msichana huyo auawe kilikuwa ni kitu kisichowezekana hata kidogo. Aliendelea kufuatilia kwa kuhisi kwamba kwa sababu baba wa msichana huyo alikuwa mfalme basi hilo lisingekuwa tatizo hata kidogo, baada ya hukumu kutolewa na baba kuridhia, hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kumuokoa msichana wake.


Alichokifanya ni kuandaa kiasi cha dola milioni moja kwa ajili ya watu ambao walikuwa na kazi kubwa ya kufanya. Akawatafuta vijana ambao walikuwa katika wakichukua mafunzo na kuwa CIA. Ilikuwa ngumu sana kuwapata lakini kutokana na kuwa na ukaribu na watu hao, hasa viongozi, akawapata na hivyo kuwapa kazi hiyo.


Walikuwa vijana wanne, mbele yao kulikuwa na kazi kubwa lakini hawakuwa na jinsi, kwa sababu kiasi kikubwa cha fedha kiliwekwa mezani, ilikuwa ni lazima wafanikishe kile walichoambiwa.


Baada ya siku mbili, wakaanza safari ya kuelekea nchini Kuwait, njiani, walitumia vitambulisho vilivyowaonyesha kwamba walikuwa katika safari ya kuelekea katika kituo cha kijeshi cha Marekani nchini humo, hivyo hawakupata tabu.

“Tutapata kila kitu kambini, msijali,” alisema Kurt, mmoja wa vijana hao.


Walipofika nchini humo, walichokifanya ni kwenda katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa nchini humo, walipofika, kwa kuwa walikuwa na vitambulisho na walijulikana kupitia Mike ambaye aliwapa taarifa mapema, wakapewa silaha ambazo wangezitumia katika safari yao ya kumuokoa msichana Aisha.


Siku zote hizo walilala hapohapo huku wakifuatilia ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Mahakamani, nao walikuwepo, kila sehemu ambayo walitakiwa kuwepo, walikuwepo.


Siku ambayo ndiyo hukumu ingetekelezwa, waliwahi asubuhi na mapema katika uwanja huo, kitu cha kwanza wakaweka vinasa sauti vilivyokuwa na nguvu mahali hapo, waliangalia huku na kule kama kuisoma ramani na kisha kurudi ndani ya gari.


Gari lao halikutoka katika eneo hilo. Ilikuwa ni vigumu kuwafahamu watu waliokuwa ndani ya gari hilo kwani lilikuwa na vioo vilivyowekwa tinted kila kona.


Watu wakaanza kukusanyika mahali hapo, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Kurt na wenzake walikuwa wakifuatilia kila kitu. Silaha zao zilikuwa mikononi mwao. Mpaka Aisha analetwa mahali hapo, tayari walikuwa wamekwishajipanga na kusikiliza kila kitu kilichokuwa kikiendelea kupitia vinasa sauti walivyokuwa wameviweka.


“Vipi! Tuanze sasa hivi?” aliuliza kijana mmoja.


“Subiri kwanza...”

“Ila watamuua, si unasikia ndiyo wanakwenda hatua nyingine!”

“Wala msijali! Hatuwezi kuchelewa hata kidogo!” alisema Kurt huku akiwa na uhakika kwamba wasingeweza kuchelewa.


Baada ya mtu mmoja kuhesabu moja mpaka mbili, ndipo Kurt aliposhusha kioo na kupiga mabomu matatu ya gesi, watu walipoona moshi mkubwa ukitanda, wakashindwa kufanya walichotaka kufanya, hapohapo wakaanza kukimbia kwani tayari sehemu hiyo ilionekana kuwa si salama tena.


“Nyie endeleeni kupiga, acha nikamchukue...” alisema Kurt huku akiufungua mlango wa gari na kutoka.


“Sawa! Wewe nenda, tutakulinda,” alisema kijana mwingine na Kurt kuteremka, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea kule alipofukiwa Aisha.


Alipomfikia, akamfukua, akamchukua na kumpeleka garini. Safari ikaanza mara moja.


****


Ilikuwa ni lazima waondoke nchini Kuwait kwa kutumia usafiri wowote ule lakini si kubaki mahali hapo. Ndani ya gari, bado msichana Aisha alikuwa akijiuliza juu ya watu waliokuwa humo, hakujua walikuwa wakina nani na kwa nini waliamua kumuokoa kutoka katika kifo.

Gari liliendeshwa kwa kasi, walichomwambia Aisha ni kwamba walikuwa wakitaka kuelekea nchini Iraq. Aisha ndiye alikuwa muelekezaji kwamba wapi walitakiwa kupita mpaka kufika nchini humo.


Njiani, hawakutaka kuendesha kwa kasi sana kwa kuogopa kugundulika, waliendelea mpaka walipofika sehemu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya watu, hapo ilikuwa ni kwenye Soko Kuu la Jahra ambalo asilimia kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali Kuwait walipendelea kufika hapo kwa ajili ya kufanya manunuzi yao.


“Nyie ni wakina nani?” aliuliza Aisha baada ya ukimya wa muda mrefu.


“Sisi?”

“Ndiyo!”


“Huwezi kutufahamu!”


“Kwa nini? Nataka niwafahamu na kwa nini mmeniokoa,” alisema Aisha.


“Kwa sababu tulitumwa.”

“Na nani?”


“Usijali! Utajua tu.”


Hawakutaka kuzungumza kitu kingine chochote kile, walichokitaka ni kufika kule walipoambiwa wafike na mambo mengine kuendelea. Tayari walikuwa wamekwishafika Khaitan, wakaambiwa wageuze, wasitumie tena mpaka wa kuingilia Iraq kwani tayari serikali ilishaagiza kufungwa kwa mipaka hiyo, hivyo walitakiwa kutumia boti.


“Amesemaje?”


“Tutumie boti. Hivi hapa tunaweza kupita wapi mpaka tufike baharini?’ aliuliza Kurt.


“Kama kilometa mia nane hivi, hapa ni Khaitan, kwa hiyo inatupasa turudi mpaka katika Jiji la Kuwait, huko, tutachukua njia ya kwenda Salmiya,” alijibu Aisha.


“Sawa.”

Walichokifanya ni kugeuza na kisha kuanza safari nyingine, njiani, kila mmoja alikuwa na wasiwasi, kilometa mia nane zilikuwa nyingi sana hivyo kila wakati walitulia njiani kisha kuendelea na safari.


Bado kichwa cha Aisha kilikuwa na maswali mengi, hakuwafahamu watu hao, walikuwa wageni na kitu kilichomuumiza kichwa chake ni kwamba hakujua mtu ambaye aliwatuma kuja kumuokoa.


Mawazo yake yalikuwa kwa baba yake tu, aliamini kwamba ndiye alitumia kiasi cha fedha kumuokoa kwani bado alikuwa akimpenda mno. Kuna kipindi alihisi kwamba inawezekana akawa Mike lakini kila alipokumbuka kwamba mtu huyo hakuonekana kujali sana hata kipindi alichomwambia kwamba atauawa, hakufikiria kama angeweza kufanya kitu kama hicho.


Safari iliendelea zaidi, walipobakiza kilometa kama mia tano kabla ya kuingia katika Jiji la Kuwait, wakaona magari mengi yakiwa yamesimama kando ya barabara na polisi wakilikagua kila gari lililopita mahali hapo.


Wakashtuka, hawakuwa wamefikiria kama kungekuwa na msako kiasi hicho, hawakutaka kujiuliza sana, walijua tu kwamba ni msichana Aisha ndiye aliyekuwa akitafutwa. Alichokifanya Kurt ni kuwasha redio.


“Wanasemaje?” aliuliza Kurt huku akimwangalia msichana Aisha.


“Mungu wangu!”


“Nini?”

“Mipaka yote imefungwa na ulinzi umeimarishwa, natafutwa kwa udi na uvumba huku kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimeandaliwa,” alijibu msichana Aisha.


Kwanza wakaangaliana, wakapata jibu juu ya foleni ile iliyokuwepo. Kuvuka mahali hapo pasipo kukaguliwa lilikuwa jambo gumu sana, hivyo wao kama majasusi walitakiwa kufanya kitu fulani.


“Tufanyeje?” aliuliza Shawn.


“Subiri, hebu nipeni dakika kadhaa,” alijibu Kurt, akaegemea usukani, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alijifikiria ni kwa jinsi gani wangeweza kuvuka mahali pale.


Sehemu ile ilionekana kuwa na msako mkubwa, polisi, wenye bunduki na mbwa walisimama kila kona. Walikuwa makini mno kwa kila gari lililokuwa likipita mahali hapo.


Watu wengine waliamriwa washuke garini na wao kupekua gari, wengine walipelekwa pembeni kabisa. Mtu aliyekuwa akihitajika mahali hapo alikuwa mmoja tu, msichana Aisha ambaye kwa kipindi naye alikuwa safarini kuelekea baharini, kupanda boti na kuelekea nchini Marekani.


****


Taarifa za uvamizi uliofanyika nchini Kuwait ukamfanya kila mtu kuashangaa, hawakuamini kama kweli kungetokea na tukio kama lile kwani hapo kabla, halikuwahi kutokea hata siku moja.


Nchi nyingi za Kiarabu zilikasirika, kwao, kuchukuliwa kwa msichana Aisha ilionekana kuwa aibu. Alifanya kosa kubwa, hakutakiwa kusamehewa hata mara moja na hata ule uvamizi uliofanyika wa kumuokoa, haukukubalika.


Ilichokifanya nchi ya Kuwait ni kuhakikisha mipaka ya nchi yote inafungwa, si ya kutoka nchini tu bali hata ya ndani kwa ndani, yaani mkoa kwa mkoa, jiji kwa jiji ilitakiwa kufungwa.


Picha nyingi za Aisha zikachapishwa na kubandikwa barabarani na kwenye vituo vya mabasi, alionekana kuwa mtu mbaya ambaye hakustahili msamaha wowote ule, iwe isiwe ilikuwa ni lazima apatikane na kurudishwa katika sehemu ya hukumu na mambo mengine kuendelea.


“Tunatoa saa ishirini na nne, awe amepatikana,” alisema waziri mkuu.


Hilo suala mfalme Sabah halikumuhusu hata mara moja, kila mtu nchini Kuwait alihisi kwamba yeye ndiye alikuwa nyuma ya kila kitu japokuwa watu waliomuokoa hawakuwa wameonekana. Wapo wengine waliosema ni Wazungu, wengine wakasema ni Waarabu wenzao lakini wengine walikwenda mbali na kusema kwamba msichana huyo aliokolewa na Waisrael.


“Tutajua tu ukweli!”


Suala la Aisha likawa gumzo. Shirika la kijasusi la nchini Kuwait likaamua kuchukua video ya kila kitu kilichotokea katika uwanja ule. Walifanikiwa kuliona bomu la gesi likidondoshwa katika uwanja huo ila hawakujua mahali lilipotoka.


Walituliza vichwa vyao lakini hawakufanikiwa kuona kitu chochote kile. Baada ya kuendelea kukaa na kuangalia, kwa mbali wakawaona watu wawili wakikimbia na kuelekea katika gari ambalo nalo hawakuliona vizuri kutokana na moshi kutapakaa kila kona.


Hawakuwa na shaka kwamba watu hao walikuwa ni Aisha na mtu aliyekuja kumchukua. Walichanganyikiwa, ingekuwa bora hata kuliona hilo gari, au mtu kujua alikuwa mtu kutoka nchi gani, kilichoagizwa ni kufungwa kwa mipaka yote huku kwa mtu ambaye angefanikisha kupatikana kwake, angezawadia kiasi kikubwa cha fedha.


“Ni lazima apatikane, cha msingi anzeni kufunga mipaka ya kila kona,” alisema mkuu wa polisi hapo Kuwait, kamanda Abdul Aziz.


“Hakuna tatizo mkuu!”


“Na hakikisheni hata hao watu waliomtorosha wanapatikana pia,” aliongezea.


“Hakuna tatizo mkuu!” walijibu polisi kisha kupiga saluti na kutoka ndani ya ofisi ya kamanda wao.





Kama fedha alikuwa nazo hivyo hakutaka kuona mpenzi wake akifa au hata akipata tatizo lolote lile, alichokifanya ni kujipanga kuhakikisha Aisha anafika salama nchini Marekani na mambo mengine kuendelea.


Alichotaka kutumia ni jeshi la Marekani ambalo lilikuwa nchini humo. Alitoa kiasi kikubwa cha fedha na kuzungumza na mkuu wa jeshi aliyekuwa katika kambi huko nchini Kuwait, alizungumza naye kwamba alihitaji msichana wake apewe ulinzi wa uhakika mpaka anafika salama nchini Marekani.


Kamanda huyo akamuahidi kwamba kila kitu kingekuwa poa, kama ni kumlinda, angemlinda mpaka anaingia nchini Marekani hivyo akampa kiasi cha dola milioni moja ambazo kwa Tanzania zilikuwa ni zaidi ya bilioni mbili.


Meli kubwa ya kijeshi ikaandaliwa, ilikuwa ni lazima msichana Aisha achukuliwe na kuingizwa humo, ila kabla ya kufika huko, ilikuwa ni lazima aingizwe katika boti moja ambayo ingepelekwa mpaka katika boti nyingine ya kifahari ambayo ndiyo ingekwenda mpaka katika manowari ya kijeshi ya jeshi la Marekani.


Alichokifanya Mike ni kuwasiliana na Bwana Malik Khalifa, bilionea mkubwa wa mafuta nchini humo na kumwambia kwamba alikuwa akihitaji boti ya kifahari hivyo kama litakuwa jambo la msingi amkodishe kitu ambacho hakikuwa na tatizo lolote lile.


“Dola laki tano, zipo?” aliuliza Bwana Khalifa.


“Zipo! Wewe tu.”


“Ila nataka niweke masharti pia,” alisema Mike.


“Yapi hayo?”

“Kusiwe na mtu mwingine zaidi ya nahodha mmoja,” alisema Mike.


“Hakuna tatizo! Ila boti yangu itakuwa kwenye usalama?” aliuliza.


“Bila shaka! Hutakiwi kuhofia chochote kile, na kama bahati mbaya kukitokea tatizo, naomba nihusike katika matengenezo na malipo mengine,” alijibu Mike kwa kujiamini.


Hakukuwa na kingine kilichofanyika zaidi ya malipo kufanyika na moja kwa moja mzee Khalifa kuagiza boti yake ya kifahari, yenye kila kitu ndani na kwenda huko tayari kwa kumchukua mtu ambaye hakuambiwa ni nani.


Wakati Mike akifanya mipango yote hiyo, tayari alikwishawasiliana na Kurt na kumwambia kuhusu mpango uliokuwepo kwani alijua fika kwamba watu hao wangetaka kwenda nchini Marekani kwa kutumia gari kupita katika nchi nyingine mpaka China ambapo wangechukua ndege kitu ambacho alikuwa na uhakika kwamba wangeweza kukamatwa njiani.


****


Kurt akakiinua kichwa chake na kuwaangalia watu wote waliokuwa ndani ya gari hilo. Yeye ndiye aliyekuwa akisubiriwa, kila mtu alitaka kujua nini kilimjia kichwani mwake ili wafanye kila liwezekanalo na kutoka mahali hapo.


“You are a pregnant woman,” (Wewe ni mwanamke mjauzito) alisema Mike huku akimwangalia Aisha.


“What do you mean?” (Unamaanisha nini?)


“You are pregnant, you are going to have a baby after few minutes,” (Una mimba, unakwenda kujingua mtoto dakika chache zijazo) alisema Mike, kila sentensi aliyoongea mahali hapo, hakukuwa na aliyeielewa.


Alichokifanya ni kuinama chini ya kiti chake, kule kulikuwa na mfuko mkubwa ambao walitumia kubebea nguo nyingine mara baada ya kutoka katika eneo la tukio kwani wasingeweza kwenda na nguo hizohizo.


Alichokifanya ni kutoa nguo hizo na kisha kisha kumpa Aisha aziweke kwenye tumbo lake na kujifanya mwanamke mjauzto aliyekuwa katika hatua za mwisho kabisa kujifungua.


“Nitaweza?” aliuliza Aisha.


“Utaweza tu, ila sasa....”


“Ila nini?”


“Nataka kupewa maelekezoyote, itakuwaje kama nikionekana?” aliuliza Aisha.


“Sikiliza, utakapokuwa kwenye maumivu, wala usiuonyeshe uso wake, jifanye kama una maumivu makali, upo kwenye uchungu huku ukilalamika, ukifanya hivyo, tutafanikiwa. Shawn, huyu atakuwa mke wako,” alisema Kurt.


“Unasemaje?”

“Usihofu, mi kwa muda tu.”


Hakukuwa na cha kusubiri, kwa sababu walikuwa kwenye foleni ya kusubiri kupekuliwa, Kurt akamwambia Aisha afanye kama alivyomwambia, akachukua nguo na kuziweka kwenye tumbo lake kisha kuchukua maji na kummwagia kichwani kidogo ili yatakapoanza kutiririka lionekane kama jasho.


“Tayari?”

“Ndiyo!”


Alichokifanya Kurt ni kutoka katika foleni ile, mbele yao kulikuwa na magari zaidi ya ishirini, polisi wote walioliona gari hilo likitoka na kwenda kule walipokuwa walibaki wakishangaa, walichokifanya ni kuandaa bunduki na mbwa wao.


Kurt hakutaka kuchelewa, alitakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu kinakuwa kama kinavyotakiwa. Alipofika kwa polisi wale, akashusha kioo na kuanza kuwaangalia.


“Naomba mtusaidie, tusaidieni huyu mwanamke atakufa,” alisema Kurt huku akionekana kuwa na haraka na wasiwasi umemjaa.


“Kuna nini?”

“Yupo kwenye hali mbaya, anakufa, anataka kujifungua, yupo kwenye hatua za mwisho kabisa,” alisema Kurt huku akilichezesha gari lile, yaani kwenda mbele kidogo na nyuma kidogo kuonyesha kwamba walikuwa na haraka na kweli mwanamke huyo alihitaji msaada.

Polisi wawili wakachungulia ndani ya gari, macho yao yakatua kwa Aisha, hawakuweza kuuona uso wake kwani kila wakati alikuwa akiuficha huku akilalamika kwa maumivu makali ya tumbo ambalo lilionekana kuwa kubwa.


Waarabu walithamini hali za wagonjwa, kitendo cha kumwona Aisha akiwa kwenye hali ile, wakachanganyikiwa, na kwa jinsi Kurt alivyojifanya kuwa na haraka ya kuruhusiwa na kuondoka, wakazidi kuchanganyikiwa zaidi na kuamini kwamba kweli mwanamke huyo alikuwa mjauzito.


“Tunaomba tupite jamani, damu zishaanza kumtoka,” alisema Kurt huku akiwaangalia polisi wale nyusoni mwao.


Ilikuwa ngumu kuamini kwamba Aisha hakuwa na mimba, maigizo waliyoyafanya mahali hapo, yalithibitisha kwamba watu hao walikuwa majasusi waliosomea.


Polisi hawakujua hilo, walichokifanya ni kuruhusu gari hilo lipite haraka iwezekanavyo ili liwahi katika Hospitali ya Khatourm ambayo haikuwa mbali na hapo walipokuwa.


Kurt akakanyaga mafuta na kuondoka mahali hapo kwa mwendo wa kasi. Hakukuwa na aliyeamini kwamba wangeweza kuvuka kirahisi namna hiyo. Baada ya kufika mbele kabisa, Aisha akarudi katika hali yake ya kawaida na kutoa nguo zile.


“Tumevuka...” alisema Kurt huku akionyesha tabasamu, tayari gari hilo likaanza kuingia katika jangwa dogo la El Shimareek lililokuwa Mashariki mwa jiji la Kuwait.


“Siamini...”


“Amini! Upo na watu wenye akili nyingi, ni lazima tutafika Marekani!” alisema Kurt.


“Marekani?”

“Ndiyo! Ooh! Samahani, hatukukwambia aliyetutuma,” alisema Kurt.


“Nani aliwatuma?”

“Mike!”

“Mike?” aliuliza Aisha huku akionekana kushtka.


“Ndiyo! Amesema ni lazima tukufikishe kwake kwa gharama zozote zile, hayupo tayari kukuona ukiuawa,” alisema Kurt huku akimwangalia Aisha machoni.


Moyo wa Aisha ukanywea, hakuamini kusikia kwamba mpenzi wake, aliyekuwa na mimba yake, Mike ndiye aliyefanya mipango yote hiyo. Kwa kuonyesha hivyo tu, akagundua jinsi mwanaume huyo alivyokuwa na mapenzi mazito kwake.


Akashindwa kuvumilia, alikuwa na furaha mno, hapohapo machozi ya furaha yakaanza kumtiririka mashavuni mwake.


“Mike ndiye aliyefanya hivi?” aliuliza Aisha.


“Ndiyo! Anakupenda sana, ni lazima tufanye kazi yake,” alisema Kurt huku safari ikiendelea.


Safari iliendelea zaidi, walipita katika jangwa hilo ambalo lilikuwa na lami mpaka walipopofika katika mji mwingine wa El Salmiya ambapo tayari muda ulikuwa umekwenda na hivyo kutakiwa kupumzika hapo.


Walichokifanya ni kuchukua vyumba katika hoteli moja huku wakiingia na Aisha ndani ya hoteli hiyo na yeye kuchukua chumba huku akiwa amevalia baibui na nikabu na kujitambulisha kama mfanyabiashara kutoka Iraq.


Hakukuwa na mtu aliyehofia chochote kile wala kumgundua msichana Aisha mpaka kipindi alipokwenda chumbani kwake. Huko, kitu cha kwanza ni kutulia kitandani na kuanza kuyafikiria maisha yake.


Mpaka kipindi hicho, bado hakuamini kama kwelia linusurika kuuawa kwa kupigwa mawe, hapo ndipo aipoamini kwamba mpenzi wake, Mike alimthamini na jicho lake lilikuwa kwake.


“Nashukuru kwa kuniokoa,” alisema Aisha wakati akizungumza kwenye simu.


“Usijali mpenzi. Bado ninakuhitaji wewe na mtoto wangu, siwezi kuruhusu jambo baya lolote kwenu,” alisikika Mike.


Usiku wa siku hiyo Aisha na wanaume wale wakalala ndani ya hoteli hiyo. Siku iliyofuata, akaamka tayari kwa kujiandaa. Hakukumbuka kuswali, alichokifanya ni kuelekea bafuni, akaoga, alipomaliza, akarudi chumbani na kuanza kujiandaa huku tayari ikiwa ni saa kumi na mbili asubuhi.


“Ngo ngo ngo ngo...” ulisikika mlango ukigongwa kwa nguvu.


Aisha akashtuka, hakujua ni nani alikuwa akigonga mlango kwa nguvu kiasi hicho. Kwanza akaogopa kwa kuhisi kwamba inawezekana ni mtu mbaya hivyo akasubiri. Baada ya kusikia mtu akiita na sauti ilikuwa ni ya Kurt, akaenda kuufungua mlango.


“Kuna nini?” aliuliza Aisha huku akimwangalia Kurt usoni.


“Kuna polisi wamekuja, wapo wengi na wamezingira hoteli,” alijibu Kurt.


“Unasemaje?” aliuliza Aisha huku akirudi chumbani, akaelekea dirishani na kuchungulia, kweli, idadi kubwa ya polisi walikuwa wamefika hotelini hapo, walikuwa na bunduki, walitaka kumchukua Aisha, walisikia taarifa kwamba msichana huyo alikuwa humo, na walikuwa mahali hapo kwa ajili yake, Aisha akabaki akiwa na hofu kubwa.


“Tutaondoka vipi?” aliuliza Aisha huku akiwa amechanganyikiwa kama kichaa, macho yake yakaanza kuwa mekundu.


Msako wa kumtafuta Aisha bado ulikuwa ukiendelea mitaani, kile kilichotokea kiliitikisa nchi ya Kuwait, na si Kuwait peke yake bali hata nchi nyingine za Kiarabu, zote zilitikisika.


Mitaani watu waliendelea kuwa makini kwani kile kiasi cha fedha kilichokuwa kimeahidiwa kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake kiliwachanganya watu wengi.


Baada ya polisi kuendelea na msako, wakapata taarifa kwamba mara ya kwanza msichana huyo na watu waliomchukua walikuwa wakielekea Khaitan lakini baadaye wakahairisha na hivyo kuanza kurudi Kuwait kwa ajili ya kuelekea katika Jiji la El Salmiya.


“Ni lazima twende huko. Kwanza walipita vipi njiani?” aliuliza mkuu wa polisi hapo Kuwait lakini hawakupata jibu.


Kilichowachanganya ni namna ya watu hao walivyojiachia njiani kwenda Khaitan mpaka kurudi tena Kuwait na kujiandaa kwenda huko El Salmiya. Walipita vipi katika vizuizi vilivyokuwa njiani na wakati kote huko kulikuwa na polisi waliokuwa wakipekua kila gari lililopita.


“Ilikuwaje mpaka wakapita hapa?” aliuliza mkuu wa polisi wa jiji hilo la Kuwait.


“Sina uhakika kama walipita hapa, tulipekua kila gari,” alijitetea polisi mmoja.


“Una uhakika?”

“Ndiyo! Hakukuwa na gari ambalo hatukulipekua!” alijibu.


“Sasa walipitaje?”

“Sidhani!”


Polisi waliokuwa hapo walibisha, kila walipokumbuka vizuri kama kulikuwa na gari lililopita pasipo kulikagua, hakukumbuka kufanya hivyo. Waliendelea kujiuliza na mwisho wa siku kukumbuka kwamba kweli kulikuwa na gari ambalo lilipita, hawakulikagua ndani bali waliwaona wanaume wakiwa na mwanamke mjauzito.


“Mlimwangalia mwanamke huyo?”

“Wapi?”

“Usoni!”


“Hapana! Alikuwa kwenye maumivu makali!” alijibu polisi.


“Na hao wanaume walikuwaje?”

“Ni Wamarekani!”

“Mungu wangu! Ndiyo wenyewe!”

“Unasemaje?”


Hakukuwa na cha kusubiri mahali hapo, polisi walionekana kuwa wapumbavu, kisa mwanamke kuwa mjauzito, hiyo haikustahili kabisa kuliruhusu gari hilo lipite kiholela pasipo kukaguliwa.


Walichokifanya ni kuingia garini na kuondoka. Sehemu pekee ambayo walijua kwamba watu hao walikuwa wakielekea ilikuwa ni jijini El Salmiya tu. Njiani, dereva aliendesha kwa mwendo wa kasi, tayari giza liliashaanza kuingia, kitu walichokuwa wakimuomba Mungu ni kuvuka salama katika jangwa dogo la El Shimareek ambalo kwa nyakati za usiku ambapo huwa na baridi kiasi, upepo huupelekea mchanga wa jangwa hilo barabarani na kuifunika barabara hiyo.


Ndani ya dakika chache walikuwa katika jangwa hilo, walichokiona kiliwafurahisha kwani japokuwa upepo ulikuwa ukipiga lakini changa haukuweza kuifunika barabara hiyo.


Safari iliendelea, walipofika katika Jiji la El Salmiya huku tayari ikiwa ni saa mbili usiku, kazi ikawa kutafuta hoteli ambayo walikuwa na uhakika kwamba watu hao walielekea.


Hoteli ya kwanza kabisa kufika ilikuwa ni Paradise, moja ya hoteli kubwa huko El Salmiya, walipofika hapo, swali la kwanza kabisa lilikuwa ni kuuliza kama kulikuwa na Wamarekani wamefika hapo, wakaambiwa hawakufika.


Waliendelea kutembelea hoteli mbalimbali na mwisho wa siku kufika katika Hoteli ya Sultan ambapo baada ya kuulizia wakaambiwa kwamba ndiyo, kulikuwa na Wamarekani watatu walifika hapo kupanga huku wakiwa na msichana wa Kiarabu.


“Ndiyo, walifika hapa saa mbili zilizopita!” alijibu mhudumu.


“Una uhakika?”


“Ndiyo!”


Walichokifanya polisi hao ni kuwasiliana na polisi wenzao, wakawapa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea na hivyo kutakiwa kufika mahali hapo. Kwa kuwa hawakutaka kugundulika kama walikuwa hapo, wakawaambia kwamba mara watakapokuwa wakija, wasiwashe ving’ora kwani wangewashtua watu hao.


“Hakuna kuwasha ving’ora, kuweni makini sana katika hilo,” alisema polisi huyo.


“Sawa mkuu!”


Baada ya dakika tano, polisi wengine wakafika hotelini hapo, walifanya kama walivyoambiwa kwamba hawakutakiwa kuwasha ving’ora vya magari yao. Walipofika, wakachukua bunduki zao na kujiandaa kwa kile ambacho wangeambiwa wakifanye.


Hakukuwa na muda wa kutafuta vibali vya kufanya upekuzi, walitumia vyeo vyao kuanza kupekua kila chumba. Walianzia vya ghorofa ya chini kabisa, vyumba vyote, hawakukuta mtu. Hawakukubali, wakapanda juu, kote huko hawakukuta mtu.


Walichanganyikiwa, hawakuamini kama walikuwa wakienda kushindwa. Waliambiwa kwamba kulikuwa na Wamarekani watatu waliingia wakiwa na msichana, sasa iweje waanze kupekua kila chumba wasiwaone watu hao?


Hawakutaka kukata tamaa, walichokifanya zaidi ni kuingia mpaka vyooni, kote huko, kila walipopita hawakuambulia kitu, watu hao hawakuonekana hata kidogo.


Hilo liliwachanganya sana, kila walipotaka kuondoka mahali hapo, ilikuwa vigumu sana, mioyo yao ilikataa kabisa hali iliyowapa uhakika kwamba watu hao walikuwa humo. Sasa ni sehemu gani walipokuwa? Kila walipojiuliza, walikosa majibu.


“Vipi?” aliuliza mkuu wa polisi.


“Hakuna mtu.”

“Hakuna mtu?”

“Ndiyo mkuu!”

“Mmeangalia kila vyumba?”

“Ndiyo! Tena hasahasa hivi walivyochukua wao, hakuna kitu,” alijibu polisi huyo.


Kuaminika ilikuwa ngumu sana, walikuwa na uhakika kwamba watu hao walikuwa ndani ya hoteli hiyo, sasa iweje polisi hao waseme kwamba waliwatafuta kila kona ikiwemo ndani ya vyumba walivyofikia lakini waliwakosa?


Mkuu wa kituo hakutaka kukubali hata mara moja, alichokifanya, yeye kama polisi wengine naye akaingia ndani ya vyumba hivyo kupekua, chumba kwa chumba, bafu kwa bafu, hawakutakiwa kuacha sehemu yoyote ile.


“Watapatikana tu,” alisema polisi huyo huku wakiendelea kupekua kwenye kila chumba.


****


Hali ilikuwa ni ya hatari sana, nje kulikuwa na polisi na walitakiwa kuondoka mahali hapo haraka iwezekanavyo. Mtu aliyekuwa akihitajika alikuwa Aisha tu, huyo ndiye alikuwa mzigo ambao wao waliutaka lakini hata hao polisi waliutaka pia.


Walikusanyana ndani ya chumba kile na kupanga mikakati ya kuondoka hotelini hapo. Silaha walikuwa nazo, lilikuwa jambo jepesi sana kutumia silaha lakini kutokana na hali iliyokuwepo, hasa wingi wa polisi wale, hakukuwa na uwezekano wa kufanya hivyo.


“Ni lazima tushuke chini,” alisema Kurt.


“Tutashuka vipi?” aliuliza Shawn.


“Subiri!”


Alichokifanya Kurt ni kuchungulia nje kupitia dirishani, alitaka kuangalia kama kulikuwa na uwezo wa kutoka ndani ya chumba kile. Chumba cha tatu kutoka hapo walipokuwa kulikuwa na bomba moja la maji ambalo lilishuka chini, iwe isiwe, ilikuwa ni lazima watumie bomba lile kushukia chini.


“Ni lazima tushuke kupitia bomba lile,” alisema Kurt.


“Lile kule?”

“Ndiyo!”


Kwao halikuwa tatizo lakini kwa Aisha ilikuwa ni tatizo kubwa. Walichotakiwa kufanya kilikuwa ni kutoka hapo chumbani kupitia dirishani, wapite kupitia ukuta ule, nje nje, dirishani kwa dirishani mpaka watakapolifikia lile bomba na kuteremkia chini.


“Nitaweza kweli?” aliuliza Aisha.


“Usijali! Utaweza tu,” alisema Kurt.


Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, walichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile na kutoka nje kupitia dirisha lile. Mtu wa mbele alikuwa Kurt, aliyefuata alikuwa Aisha, aliyefuata alikuwa Shawn na wa mwisho alikuwa Sam.


Waliambaa katika ukuta ule huku wakiwa wamefunga dirisha. Aisha aliogopa, kule alipokuwa akipitishwa, tena ghorofani kulionekana kuwa na hatari kubwa lakini hakutaka kubaki.


Aliyafumba macho yake kwa kuhisi kwamba kama angeyafumbua basi angejisikia kizunguzungu na kuanguka chini. Waliendelea kuambaa mpaka walipolifikia bomba lile ambalo Kurt akalidandia, wengine wakafuata na kuanza kuteremka chini.


Japokuwa polisi walikuwa wamezunguka hoteli ile lakini hawakuzunguka katika upande ambao bomba lile lilipokuwa kwani chini ya bomba lile kulikuwa na choo, mbali na hiyo, karibu na choo kile kulikuwa na sehemu iliyokuwa na nyaya nyingi za umeme ambazo zilitumika katika hoteli ile.


Waliteremka kwa kasi kubwa huku wakimsisitizia Aisha afanye hara, kasi yao ya kushuka kupitia bomba hilo walitumia dakika tano tu, wakawa chini na hivyo kuuanza kuelekea katika choo kidogo ambacho kilionyeshwa kutokutumiwa mara kwa mara.


“Tuingieni chooni, hakuna usalama, huko, tutaruka kupitia dirishani na kwenda upande wa pili,” alisema Kurt na wote kufanya kama walivyoambiwa.


Wakaingia ndani ya choo kile, hakikuwa kisafi, kilitelekezwa. Ndani ya choo kile kulikuwa na kidirisha kidogo kilichokuwa na nondo zilizochoka, hakukuwa na muda tena, alichokifanya Kurt ni kuanza kuzipiga nondo zile, zikachomoka na hivyo kubebana na kuanza kutoka nje.


“Kuna nini huko?” aliuliza Shawn.


“Kuna nyaya za umeme tu, kule mbele naona kuna ukuta wa hoteli,” alijibu Shawn.


“Na nyaya zinapitika?”

“Ndiyo! Ila tunatakiwa kuwa makini mno,” alijibu Kurt.


“Basi twendeni hivyohivyo, haina jinsi.”


Kurt akarukia upande wa pili, Shawn na Sam wakambeba Aisha na hatimaye naye akapita katika dirisha lile na kulrukia chini. Kilichoendelea ni kuanza kuelekea kule kulipokuwa na ukuta, tena huku wakipita katikati ya nyaya za umeme.


“Inatakiwa kuruke ukutani,” alisema Kurt.


“Ila kuna nyaya za umeme.”

“Hakuna tatizo, tuzime umeme.”


Walikuwa majasusi ambao walifahamu mambo mengi, wanapokuwa kambini, hufundishwa masuala ya kompyuta, jinsi ya kucheza na programming na software kwa ujumla, mbali na mambo ya kompyuta, pia walifundishwa kuhusu umeme.


Kurt akakifuata chombo kilichokuwa kimekusanya nyaya nyingi za umeme na kuanza kuzikatakata nyaya muhimu kwa kutumia kisuu chakke kidogo kilichokuwa na plastiki hasa zile nyaya zilizokuwa zikipitisha umeme.


Mara umeme ukakatika hotelini. Hakuishia hapo kwani baada ya umeme kukatika tu, jenereta likajiwasha. Kwa haraka sana akalisogelea na kisha kulizima.


“Tuna sekunde thelathini kuruka ukuta ule,” alisema Kurt.


“Sawa. Tufanyeni haraka.”


Ndicho walichokifanya, mtu wa kwanza kupanda juu alikuwa Kurt, alipofika juu, akazing’oa zile nyaya zilizokuwa zimepitishwa na kisha kuanza kumvuta Aisha. Walifanya hivyo kwa kusaidiana mpaka wote wakawa juu ya ukuta ule, wakarukia upande wa pili ambapo kulikuwa ni ufukweni, walichokifanya ni kuanza kuambaaambaa huko.


Walikuwa wakikimbia kwa kasi kuelekea upande wa Kaskazini, kulikuwa na giza lakini hawakutaka kusimama, ilikuwa ni lazima watoroke kwani kesho yake asubuhi, boti ya kifahari ilitakiwa kufika mahali hapo, iwachukue na kuondoka zao.

Wakati wakiwa kwenye kasi, mara wakasikia mlio wa risasi moja ikipigwa hewani, hawakujua ni nani alikuwa ameipiga kwani giza lililokuwepo mahali hapo halikuwapa uwezo wa kuona kilichokuwa mbele.


“Simameni hapohapo,” ilisika sauti ya mwanaume mmoja ambaye hawakuwa wakimuona, wakasimama.


Ghafla wakatokea wanaume wawili waliokuwa na bunduki, wakaanza kuwasogelea, walipokuwa mbali kama hatua nane, wakawaambia walale chini, harakaharaka wakalala.


“Nyie ni wakika nani?” aliuliza mwanaume mmoja kwa sauti ya juu.


“Wakimbizi...tumetoka Iran,” alijibu Aisha hata kabla Kurt hajajibu.


“Kwa nini mnapitia baharini?” aliuliza mwanaume yule huku akianza kusogea kule walipokuwa wamelala.


“Tumeamua, tunaogopa kurudishwa nyumbani! Tusaidie ndugu zako,” alisema Aisha huku akijifanya kulia.


“Na hawa ni wakina nani?”

“Kaka zangu!”


Jamaa huyo hakuishia hapo, akasogea zaidi na kumgusa Kurt kwa bunduki yake. Kurt akanyamaza, hakutaka kuzungumza kitu, alikuwa akimhesabia hatua tu.


"Tunaondoka, nadhani hautorudi tena huku," alisema Sam huku akimwangalia Aisha ambaye uso wake ulikuwa na tabasamu pana.

"Na sitotaka kurudi tena, hata kama nikifa, ni bora kuzikwa hukohuko," alisema msichana huyo huku tabasamu lake likiendelea kuwepo usoni mwake.

****

Hali ya mawingu haikuwa nzuri hata kidogo, anga ilichafuka, hakukuwa na amani hata kidogo. Marubani wawili waliokuwa wakiiendesha ndege hiyo walichanganyikiwa, hawakuamini kama kweli anga hiyo ilichafuka kiasi hicho.


Walifanya kazi ya urubani kwa zaidi ya miaka ishirini, hata anga ilipokuwa ikichafuka kwa kujaa mawingu huku mvua iliyoambatana na upepo mkali inaponyesha, hawakuwa wakiogopa lakini kwa siku hiyo, hali ilionekana kuwa tofauti kabisa.


Radi zilikuwa zikipiga kila kona, waliogopa, walihisi kwamba ndege hiyo ingepoteza muelekeo, walijitahidi kuiweka sawa kwani upepo mkali uliokuwa ukivuma ulikuwa ukiiyumbisha ndege ile kupita kawaida.


Tayari hali ya hatari ikaanza kuonekana, walichokifanya ni kuitoa ndege ile kutoka katika usawa wa nchi kavu na kuipeleka katika usawa wa bahari ya Atlantiki.


Hali ya hewa haikutulia, siku hiyo ilionekana kuwa na mkosi kwao, juhudi zao za kuiweka sawa ndege ile zilikuwa zikiendelea zaidi, mbaya zaidi, kitu kilichowatisha ni kuona injini moja ya ndege ile ikianza kuzima na kuwaka mara kwa mara.


"Vipi?" aliuliza rubani mmoja.


"Injini inazima na kuwaka, Mungu wangu! Tuombe Mungu, hali hii sijawahi kuiona tangu nazaliwa," alisema rubani mwingine.


"Hebu tuishushe ndege chini kidogo, inaweza kusaidia," alisema rubani huyo na hivyo kuanza kufanya hivyo.

Walichokuwa wakitaka ni kutoka katika wingu zito ambalo liliambatana na upepo mkali, wakaishusha ndege ile kwa chini kidogo, kama mita hamsini kutoka baharini, yote hiyo walifanya ili kuepukana na upepo huo mkali lakini cha ajabu, injini ile iliyokuwa ikiwaka na kuzima, ikazima kabisa.


"Mungu wangu! Injini imezima..." alisema rubani.

"Unasemaje?"

Huku nyuma, kila mtu alikuwa akishangaa, hali iliyokuwa ikionekana ilimtisha kila mmoja, Aisha alibaki akipiga kelele, hewa safi ya oksijeni ikaanza kupotea hivyo kuvuta mipira ya hewa safi na kujivisha midomoni na puani mwao.


"Tunakufa..." alisema Aisha huku akianza kulia.

"Hatuwezi kufa....hebu tuchukue maboya," alisema Shawn.

Hicho ndicho walichofanya, walijua kwamba kwa namna moja au nyingine marubani wale wasingeweza kuirudisha ndege ile katika hali ya kawaida kutokana na upepo mkali kuendelea kuvuma hivyo walichokifanya ni kuchukua maboya kwa kuamini kwamba kama ndege hiyo ingeanguka basi ingeangukia baharini.


"Vaa haraka Aisha...injini imezima," alisema Shawn huku akimsisitiza Aisha kuvaa boya lile. Hata kabla hawajakaa sawa, ndege ile ikaanza kushuka baharini kwa kasi, kila mtu akaogopa, tayari walikiona kifo kuwa mlangoni, baada ya sekunde kadhaa, kilichosikika kilikuwa ni puuuuu, ndege ikaangukia baharini na kuanza kuzama.


****

Mike alichanganyikiwa, hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, mara ya mwisho kuzungumza na Shawn alimwambia kwamba walikuwa ndani ya ndege wakiivuka Bahari ya Atlantiki ila kitu kilichomshangaza ni kwamba kwa kipindi hicho, simu ya mtu huyo haikuwa ikipatikana.


Hali hiyo ilimpa hofu moyoni mwake na kuhisi kwamba inawezekana kuna kitu kibaya kilichotokea, akili yake ikamwambia kwamba inawezekana kulikuwa na ajali ndiyo maana simu haikuwa ikipatikana.


Alichanganyikiwa mno, alichokifanya ni kuwasiliana na watu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK wa hapo New York ili kuona kama walikuwa na mawasiliano na marubani waliokuwa wakirusha ndege hiyo.

“Una hofu ya nini?” alisikika mwanaume mmoja akiuliza kwenye simu.

“Kuna ndege yangu ilikuwa ikitoka Dubai, nashangaa siwapati kwenye simu, kuna tatizo lolote?” aliuliza Mike huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Ndege aina gani?”

“Ndogo!”


ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Andika maoni yako hapa

  Facebook Google+ Twitter LinkedIn Tumblr Menu SKIP TO CONTENT HOME WAKUBWA TU 18+ WAANDISHI WA SIMULIZI SIMULIZI ZA SAUTI UCHAWI UPO SHUHU...