UTAJIRI WENYE UCHUNGU - 5


Sehemu Ya Tano (5)



“Aina?”


“Ultra-long-range G550.”


“Asante! Nitakupigia tafadhali.”


Simu ikakatwa, bado Mike alikuwa na hofu moyoni mwake, alikuwa na uhakika kwamba kulikuwa na kitu kilikuwa kimetokea, kila alipokaa, moyo wake ulikosa amani kabisa, hakutaka kukubali, alichokifanya nii kuondoka kuelekea huko uwanja wa ndege.


Alipofika huko, moja kwa moja akaelekea katika uongozi wa uwanja huo na kuwaambia kilichokuwa kimetokea hivyo kuchukua simu na kuwapigia watu wa mawasiliano ili waambie mahali ndege hiyo ilipokuwa kwa kipindi hicho.


“Hakuna mawasiliano...” alisema jamaa mmoja mara baada ya kujaribu kuwapigia marubani waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

“Hamuwapati kabisa?”

“Ndiyo mkuu! Labda kuna tatizo la hali ya hewa, tutaendelea kuwatafuta,” alijibu jamaa wa upande wa pili.


Mike hakutaka kuondoka mahali hapo, alitaka kufuatilia mpaka mwisho, alihitaji kufahamu ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, moyo wake ulikuwa mzito mno, kuna kipindi alisikia sauti ikimwambia kwamba ndege hiyo ilipata ajali lakini wakati mwingine alipiga moyo konde na kusema kwamba hayo yalikuwa mawazo ya kijinga tu.


Muda ulizidi kwenda mbele, baada ya saa mbili, matokeo wala hayakubadilika, yaliendelea kubaki vilevile kwamba marubani hao hawakupatikana.


“Kuna tatizo?” aliuliza Mike.


“Inawezekana ndege imepata ajali na kuzama baharini. Ngoja tuwasiliane na watu wa usalama wa majini,” alisema kiongozi wa mahali hapo na kuanza kuwasiliana.


Uchunguzi ukaanza kufanyika haraka sana, baada ya saa sita, wakapewa taarifa kwamba kulikuwa na ndege iliyokuwa imepata ajali na kuanguka baharini, walipoambiwa wataje iliandikwa vipi kwa nyuma, wakasema G550.


“Ndiyo yenyewe....” alisema Mike, akajikuta miguu ikiishiwa nguvu na kukaa chini.


Machozi yakaanza kumtoka, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alimsubiri kwa hamu mpenzi wake, alitaka kumsubiri, ampokee kwa mabusu mfululizo, sasa ilikuwaje ndege aliyopanda ipate ajali, tena katika siku ambayo kwake ilionekana kuwa ya thamani kuliko siku nyingine.


Walichokifanya ni kuwasiliana na watu wa majini na kwenda huko kufuatilia kama kuna mtu yeyote aliyepona. Mike hakutaka kukubali, hakutaka kuletewa taarifa tu bali alichokifanya na yeye kuelekea huko ili kujionea mwenyewe.


Helkopta ikaandaliwa na ndani ya dakika chache walianza safari ya kuelekea huko. Njia nzima Mike alikuwa akilia tu, hakuwa akiamini kile kilichokuwa kikiendelea kwamba mpenzi wake na mtoto wake mtarajiwa walikuwa wamekufa.


“Hivi ni kweli Aisha amekufa?” alijikuta akiwauliza watu aliokuwa nao humo ndani.


“Hatujui, lakini hakuna aliyekufa, kama kweli ilipata ajali muda saa chache zilizopita, wote watakuwa salama,” alijibu jamaa mmoja, maneno yake yalikuwa yenye kutia moyo ila kwa Mike, yaligonga mwamba.


Walichukua saa mbili mpaka kufika mahali ambapo ndege hiyo ilipokuwa imepata ajali alfajiri ya siku hiyo. Walipofika hapo, waliikuta ndege hiyo, lakini kitu cha ajabu hawakukuta mwili wa mtu hata mmoja zaidi ya nguo za marubani ambazo zilionekana kuraruliwa hali iliyoonyesha kwamba walikuwa wametafunwa na papa.


“Kitu cha kwanza ni kutafuta kiboksi cheusi,” alisema jamaa ambaye alionekana kuwa kongozi wao.


Vijana wawili waliokuwa na mitungi ya hewa safi wakaingia ndani ya maji, huko, wakaanza kutafuta hicho kiboksi cheusi ambacho waliambiwa wakitafute, wala hawakuchukua muda mwingine wakakipata na hivyo kuanza kuitafuta miili miili ya watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo.


Zoezi hilo lilikuwa kubwa na gumu, walitafuta zaidi na zaidi, walikwenda huku na kule lakini hawakuweza kuiona miili hiyo kitu kilichowafanya kuwa na wasiwasi mno.


Kati ya watu wote waliokuwa mahali hapo, Mike ndiye alionekana kuwa makini, alikuwa akiangalia huku na kule, moyo wake ulimuomba sana Mungu kwamba afanikiwe kumuona mpenzi wake lakini hilo wala halikuwezekana.


Walikaa huko kwa saa tatu lakini hawakufanikiwa kitu, hivyo Mike kuhisi kwamba mpenzi wake na watu aliokuwa amewatuma, wote walikufa katika ajali hiyo, hivyo wakarudi nchini Marekani huku akiwa na uchungu mkali moyoni mwake.


****


“Usiogope Aisha....usiogope...” ilisikika sauti kutoka kwa Shawn.


“Ninakufa...ninakufa...niokoe...” alipiga kelele Aisha.


“Huwezi kufa, hauwezi kufa....”


Walikuwa kwenye maji, walijitahidi kujitoa ndani ya ndege ile na wote wanne kuanza kuogelea. Hawakujua marubani walikuwa wapi, walichokuwa wakikiangalia kwa wakati huo ni kuyaokoa maisha yao tu.


Waliendelea kuogelea, maboya waliyoyavaa yaliwasaidia sana kuogelea. Mawimbi yalikuwa yakipiga huku na kule, kwa Shawn na wenzake hakukuwa na tatizo lolote lile lakini kwa Aisha, ilibidi ashikwe ili asiweze kupelekwa na mawimbi hayo.

Waliendelea kuogelea kwa zaidi ya saa moja na nusu na ndipo kwa mbali sana wakaweza kukiona kisiwa, hawakujua kilikuwa kisiwa gani, kilikuwa kidogo sana, hivyo wakaanza kuelekea huko.


“Ni lazima twende kule,” alisema Shawn.


“Baridi litaniua...”

“Usife...huwezi kufa, jitahidi kuvumilia Aisha. Ukifa wewe, safari yetu ya kuja Kuwait itakuwa bure kabisa, vumilia,” alisema Shawn huku akiwa amemshika mkono Aisha, waliendelea kusonga mbele kukifuata kisiwa kile.


****


Hali ilikuwa mbaya kisiwani, baridi kali lilikuwa likipiga kupita kawaida, muda wote Aisha alikuwa akitetemeka, alitoka katika nchini Kuwait, moja ya nchi za kiarabu iliyokuwa na joto kali kutokana na hali ya jangwa iliyokuwepo huko.


Kwa Shawn na wenzake, hali haikuwa mbaya sana, walichokifanya ni kuelekea katika kipori kidogo kilichokuwa kisiwani humo na kisha kuchukua kuni na kurudi.


Walizungukwa na maji kila kona na kila walipoangalia, hakukuwa na dalili za meli au mtumbwi wowote ule. Walipelekwa huko bila kutaka, hawakujua Mashariki ilikuwa upande gani, Magharibi wala upande wowote ule.


Wakawasha moto kwa njia za kusaga mawe na kisha kuanza kuota moto. Hakukuwa na aliyelala, usiku mzima walikuwa mahali hapo, walichoka, njaa iliwauma lakini hawakuwa na jinsi, walikuwa wakisubiri msaada wowote ule, uwe meli, boti au chochote kile.


Siku ya kwanza ikakatika, walikuwa hapohapo kisiwani, siku ya pili nayo ikaingia lakini hakukuwa na dalili zozote zile. Walionekana kukata tamaa, wakati mwingine Aisha aliyaona mateso ya kukaa kisiwani hapo kuwa makubwa, ilikuwa ni afadhali kuuawa kule Kuwait kuliko kukutana na mateso makali aliyokuwa akikutana nayo mahali hapo.


Siku ya tatu ikaingia, napo hali ilikuwa mbaya zaidi, hakukuwa na chakula chochote kile, miili yao ikaanza kudhoofika, ikaanza kukosa nguvu kwani kama maji, walijitahidi kuyanywa hayohayo japokuwa yalikuwa ya chumvi lakini kuhusu chakula, hawakuwa na jinsi, waliendelea kubaki njaa hivyohivyo.


“Hatuwezi kuvumilia, ni lazima tuvue samaki,” alisema Shawn huku akiwaangalia wenzake.


“Hatuna nyavu!”

“Kwani kuvua samaki mpaka nyavu? Hakuna, hata kwa kutengeneza mikuki, tutaweza kuvua,” alisema.


Hicho ndicho walichokifanya, walikuwa majasusi, wenye mafunzo mengi, walifunduishwa namna ya kupambana katika kipindi kigumu kama hicho hivyo kitu walichokifanya kilikuwa ni kukata miti, wakaichonga kwa kutumia meno yao, walipoona kidogo imepata ncha kali, wakaingia baharini.


Uvuaji huo ambao ulitumika sana katika nchi zisizoendelea ndiyo walioutumia. Ulikuwa mgumu sana lakini waliweza kuufanya hivyohivyo. Siku hiyo ya kwanza ilikuwa ngumu kwao lakini wakafanikiwa kupata samaki waliowatosha na hivyo kurudi kisiwani na kuwachoma kisa kula.


Maisha yalikuwa hivyohivyo, hakukuwa na chakula kingine zaidi ya samaki ambao waliwala pasipo chumvi, hapo hawakuangalia ladha, walichokiangalia kilikuwa ni kushiba tu.

Mpaka siku ya nne inaingia, wakipigwa baridi kali nyakati za usiku lakini hakukuwa na msaada wowote ule uliokuja, waliendelea kuishi humohumo mpaka kuyazoea maisha ya humo kisiwani.


“Tutachukua muda gani mpaka kuondoka hapa?” aliuliza Aisha.


“Inategemea.”

“Na nini?”


“Na msaada tutakaoupata, kama utachukua siku kumi, tutakaa kwa siku hizo, kama utachukua mwaka mzima, hatuna jinsi,” alijibu Shawn.


Aisha alikata tamaa, alichokuwa akikitaka ni kufarijiwa na Shawn kwamba hata kama walijua kusingekuwa na msaada wowote ule lakini aambiwe tu kwamba msaada ungepatikana.


“Wiki moja imekatika, bado tupo hukuhuku kisiwani!” alisema Aisha huku mwili wake ukiwa umekonda kwa ajili ya mawazo na tabu za mule kisiwani.


“Ndiyo hivyo Aisha! Ninajaribu kuwatafuta kwenye simu, hakuna network,” alisema Shawn.


Walikuwa na simu, yenye uwezo mkubwa ambayo haikuwa ikipitisha maji, haikutumia betri la umeme bali sola hivyo ilivyofika mchana ilikuwa ni lazima kuichaji.


“Nahisi tutakufa hapa,” alisema Aisha huku akionekana kukata tamaa kabisa.

“Haiwezekani! Hatuwezi kufa hapa!”


“Tutaupata wapi msaada?”

“Sijui! Lakini kufa hapa! Haiwezekani Aisha, tutapata msaada tu.”


Wiki ya tatu ilipoingia, Aisha akaanza kujisikia vibaya, kizunguzungu kikaanza, tumbo likaanza kumuuma mno. Alilia siku nzima, Shawn na wenzake ndiyo waliokuwa wakimpoza na kumsaidia katika kila kitu.


Hakukuwa na dawa mahali hapo, walichokifanya ni kutumia mizizi ya miti iliyokuwa kisiwani hapo kama dawa za kumtibu Aisha ambaye kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, hali yake iliendelea kuwa mbaya sana.


“Vipi Shawn?” aliuliza Sam.


“Network inakuja na kukata, inakuja na kukata....” alijibu Shawn.


Hiyo ilikuwa ni saa kumi alfajiri, hawakulala usiku mzima, ni Aisha tu ndiye aliyelala tena kwa usingizi wa mang’amung’amu. Wao walikesha wakiiangalia simu ambayo ilikuwa inashika network na kupotea.


“Fanya kitu kimoja.”

“Kipi?”

“Mtumie meseji Mike.”

“Hakuna network.”

“Wewe mtumie, kama network ikija, meseji itakwenda tu.”


Hakuwa na jinsi, alichoambiwa kilikuwa sahihi kabisa hivyo kutuma meseji hiyo ambayo wala haikwenda kutokana na eneo hilo kukosekana kwa network.


****


Mike alichanganyikiwa, hakuamini kama kweli alimpoteza msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote lakini kilichomuumiza zaidi ni kupotea kwa mtoto wake ambaye angetarajiwa kuzaliwa miezi michache ijayo.

Akakosa furaha, akawa mtu wa kulia tu, kila siku akawa anaomboleza, wakati mwingine aliona kama Mungu akimuonea tu. Alitumia gharama kubwa mno kumuokoa Aisha kutoka katika kifo nchini Kuwait mpaka huko lakini mwisho wa siku, hata kabla hajaingia nchini Marekani, tayari msichana huyo alikufa njiani.

“Mungu! Mlaze mpenzi wangu mahali pema peponi,” alisema Mike.


Hakuwa na jinsi, moyo wake ulimwambia kwamba alimpoteza mpenzi wake, hakukuwa na kingine alichokifanya zaidi ya kumtaka Mungu amlinde Aisha huko alipokuwa.


Wiki ya kwanza ikakatika, hakukuwa na taarifa zozote zile, wiki ya pili ikakatika, hakukuwa na taarifa zozote kutoka huko walipokuwa. Ilipofika wiki ya tatu, tena katikati, saa mbili asubuhi akiwa ofisini kwake huku akiwa na mawazo, akasikia mlio wa meseji ukiwa umelia kuashiria kwamba kuna meseji imeingia.


Akaichukua simu yake na kuifungua meseji hiyo, akakutana na ujumbe mfupi ulioandikwa ‘WE STILL ALIVE IN THE ISLAND’ (BADO TUPO HAI KISIWANI) Mike akashtuka, alipoangalia namba, ilikuwa ni ya Shawn.




Mike akashtuka, hakuamini kile alichokiona kwamba watu aliokuwa amewatafuta kwa wiki nzima walikuwa katika kisiwa sehemu fulani. Kwanza akainuka na kuisoma vizuri meseji ile, alitaka kuona alisoma kama ilivyoandikwa au alikuwa amechanganya, akairudia na kurudia, kweli ilisema vilevile kwamba watu hao walikuwa kisiwani.


Hakujua ni kisiwa gani walichokuwepo, hakutaka kupoteza muda humo ofisini, moja kwa moja akawasiliana na watu wa baharini na kuwaambia kwamba alipokea ujumbe wa maneno kuwa watu aliowatuma walikuwa hai kisiwani.


“Wapo na huyo msichana?” aliuliza jamaa wa idara ya ulinzi wa baharini.


“Bado sijajua, nimeuliza lakini meseji haiendi, nafikiri hakuna network,” alisema Mike.


Hakukuwa na muda wa kupoteza tena, walichokifanya ni kuingia ndani ya helkopta na kuanza safari ya kuelekea huko. Njiani, kila mmoja hakujua ni kisiwa gani ambacho walikuwepo watu hao. Ndani ya Bahari ya Atlantiki kulikuwa na zaidi ya visiwa hamsini, je ni kisiwa gani walichokuwepo watu hao, hawakujua.


“Kuna zaidi ya visiwa hamsini, sasa watakuwa kisiwa gani?” aliuliza rubani.


“Nafikiri kimojawapo, hasa kile kisichokaliwa na watu,” alijibu Mike.


Ilikuwa kazi kubwa kukisia, hawakuelewa mahali walipokuwa watu hao, walichanganyikiwa, alichokifanya Mike ni kuchukua ramani iliyokuwemo ndanii ya helkopta ile na kuanza kuangalia visiwa vilivyokuwa ndani ya bahari hiyo.


Kulikuuwa na visiwa vingi kama Braza, Fogo, West Point, Sea Lion na vingine vingi lakini kati ya hivyo vyote, vilikuwa vikikaliwa na watu, hivyo huko kungekuwa na network, walichotaka kujua wao, ni kile kisiwa ambacho hakikuwa kikikaliwa na watu na ambacho hakikuwa na network yoyote ile.


“Hivyo vyote ulivyovitaja, vinakaliwa na watu,” alisema rubani.


“Sasa kipi ambacho hakikaliwi na watu?”

“Hata mimi sijui kwa kweli, wewe twendeni tu, tutaona mbele ya safari,” alisema kiongozi wa ulinzi katika bahari hiyo, Paul.

Safari iliendelea, walipita katika visiwa vingi, kulikuwa na watu wengi, hawakutaka kutua huko, hakukuwa sehemu sahihi ambayo watu waliopotea walipokuwa.


Baada ya saa nne wakiwa angani, wakafika katika kisiwa ambacho kwa mbali hakukuwa na mtu wala jengo lolote lile, wakajua kwamba inawezekana hicho ndicho kisiwa walichokuwa wameambiwa.


Harakaharaka helkopta ikaanza kuteremka, hakukuwa na mtu zaidi ya miti, kilionekana kuwa kisiwa kilichotengwa ambacho kilikuwa mbali kabisa na visiwa vingine.


Wakateremka na kuanza kuangalia huku na kule, hakukuwa na mtu yeyote yule, walijitahidi kuangalia zaidi na zaidi tena huku wakiita, hakukuwa na mtu yeyote aliyeitikia.


“Kweli watakuwa katika kisiwa hiki?” aliuliza rubani.


“Sidhani! Hebu twendeni katika kisiwa kingine, ila hiki kimetelekezwa sana mpaka network napo hakuna,” alisema Paul.


Hawakuwa na jinsi, wakaanza kupiga hatua kurudi kwenye helkopta ile, hawakuwa na uhakika kama watu hao walikuwa kwenye kisiwa hicho au la, japokuwa walitumia saa nyingi, hawakuwa na jinsi, walitakiwa kuondoka kuelekea katika kisiwa kingine.


****


“Sam...unasikia sauti helkopta?” aliuliza Shawn.


“Hapana!”


“Hebu sikiliza vizuri...”


Kwa mbali walikuwa wakisikia sauti ya helkopta kutoka katika upande mwingine kabisa, nyuma ya kisiwa hicho. Walikuwa na uhakika kwamba sauti waliyokuwa wakiisikia ilikuwa ni ya helkopta kweli lakini haikuwa katika upande waliokuwepo, ilikuwa katika upande wa pili kabisa.


Kila mmoja akawa na nguvu isipokuwa mtu mmoja tu, huyu alikuwa Aisha ambaye kwa kipindi walichokuwa humo kisiwani, hali yake haikuwa nzuri kabisa.


Walimpa mizizo kama dawa lakini hakukuwa na kilichobadilika, hali ilikuwa mbaya mno na hakukuwa na kitu chochote alichokisubiria mahali hapo zaidi ya kifo.


Kwa kasi ya ajabu Sam akatoka mahali hapo na kuanza kuelekea upande wa pili. Kilikuwa kisiwa kikubwa mno, hata alipozunguka, alichoka sana lakini hakutaka kusimama, alikimbia ufukwe kwa ufukwe huku akiita ili kama watu hao wakisikia, basi wasimame na hivyo kuwasiaidia.


“Tusaidieni...tusaidieniiiii” aliita Sam huku akikimbia kwa kasi.


Mike na wenzake tayari walikuwa wamepanda ndani ya helkopta ile, mlio wake ulikuwa mkubwa ambao uliimeza kabisa sauti ya Sam ambaye alikuwa akielekea kule walipokuwa.


Mike hakuridhika, moyo wake ulikuwa mzito mno, hakuamini kama kweli katika kisiwa hicho hakukuwa na mtu aliyekuwa akiishi, aliamini kabisa kwamba mpenzi wake na watu aliowatuma walikuwa mahali hapo.


“Moyo wangu mzito sana,” alisema Mike huku akiwaangalia wenzake.


“Kwa nini?”

“Nadhani wapo humu.”

“Hapana! Si unaona tumeangalia kote!” alisema Paul.


“Hapana! Hatujaangalia, ila kama mnataka twende kwingine, hakuna tatizo,” alisema Mike kwa sautio ya chini, moyo wake ulikuwa mzito mno.


Helkopta ikaanza kuinuka tayari kwa kuondoka mahali hapo. Macho ya Mike yalikuwa chini, hakuamini kama kweli walikuwa wakiondoka pasipo kuwaona watu hao.


Huku helkopta ikiwa imefika umbali wa mita hamsini kutoka katika kisiwa kile, kwa mbali Mike akamuona mtu akikimbia kwa kasi kuelekea kule walipokuwa wametua.


Kwanza akashtuka, hakuamini kama kweli yule alikuwa binadamu au kiumbe kingine kwani alikuwa akionekana kwa mbali kidogo. Hapohapo akawaambia wenzake kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akikimbia kisiwani hivyo wasiondoke.


“Unasemaje?”

“Kuna mtu, yule kule chini,” alisema Mike kwa hamu, alitamani hata kujirusha kutoka katika helkopta ile.


Walipoangalia chini, kweli walimuona mtu mmoja akiwa anawapungia mikono, kila mmoja akaonekana kufurahi, kwa haraka sana, hapohapo helkopta ikaanza kushushwa, hata kabla hawajafika chini, Mike akaruka.


“Sam...” alimuita mtu huyo.


Sam hakuweza kuzungumza chochote kile, alibaki kimya, alikuwa akihema kwa nguvu, mwili wake ulichoka na alikuwa amekonda. Mike akasikia maumivu moyoni mwake, machozi yakaanza kumtoka.


“Aisha yupo wapi?” aliuliza Mike huku akionekana kuwa na wasiwasi.


“Unasema?”

“Aisha yupo wapi?” aliuliza Mike, Sam akabaki kimya kwa muda, kwa jinsi alivyoonekana, hofu kubwa ilimjaa moyoni mwake. Mike akaishiwa nguvu, akakaa chini kwani jibu alilohisi ndilo alilotegemea kupokea kutoka kwa Sam.


“Aisha amekufa...” ilikuwa ni sauti pekee iliyosikika moyoni mwa Mike.


****


Mike alibaki akitetemeka, alimwangalia Sam huku sauti ile ikiendelea kusikika moyoni mwake kwamba msichana aliyekuwa akimpenda alikuwa amekufa. Sam hakujibu kitu, alikuwa amechoka na muda wote alikuwa akihema kwa nguvu.


Mike alikuwa na shauku ya kusikia jibu juu ya kile alichokuwa amekiuliza, alibaki akimwangalia mwanaume huyo, alipopumzika kwa dakika moja, akampa jibu lililompa faraja kubwa moyoni mwake kwamba msichana huyo alikuwa hai, ila alikuwa hoi.


“Unasemaje?” aliuliza Mike.


“Twendeni...” alisema Sam.


Wakaondoka na kuelekea huko aliposema Sam. Japokuwa hakuwa akipafahamu lakini Mike ndiye alikuwa mtu wa mbele kabisa, alikuwa akipiga hatua za harakaharaka, alitamani sana kumuona mpenzi wake, alimpenda kwa mapenzi ya dhati hivyo kuona akifariki dunia, kilikuwa moja ya vitu asivyopenda kabisa vitokee.


Walichukua dakika kadhaa wakafika upande wa pili, macho ya Mike yakatua kwa watu watatu akiwemo mpenzi wake ambaye alikuwa hoi chini. Kwa hatua za harakaharaka Mike akamsogelea mpenzi wake pale chini alipokuwa.


Mwili wake ulikonda mno, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa mgonjwa, pasipo kutarajia, Mike akaanza kutokwa na machozi yaliyochanganyikana na vitu viwili, cha kwanza kilikuwa ni furaha hasa baada ya kumuona mpenzi wake lakini cha pili kilikuwa ni maumivu makali hasa baada ya kumkuta mpenzi wake akiwa kwenye hali ile.


“nini kimetokea?” aliuliza Mike.


“Mimba inaweza kuharibika...”


“Unasemaje?” aliuliza Mike huku akionekana kutokuamini.


“Mimba yake ipo kwenye hali ya hatari!”


Mike alipoambiwa hivyo akachanganyikiwa, akamwambia rubani arudi kule alipokuwa, kuichukua helkopta ile na kuipeleka katika upande mwingine wa kisiwa ili wamchukue Aisha na kuondoka naye, hicho kikafanyika haraka sana.


“Aisha...Aisha mpenzi nipo hapa kwa ajili yako...” alisema Mike huku akimwangalia mpenzi wake machoni mwake.


Aisha aliyafumbua macho kwa mbali sana, alikuwa hoi, aliumwa sana na wakati mwingine alihisi kama angekufa, kidogo uso wake ukajawa na tabasamu pana.


Wala haukuchukua muda mrefu, helkopta ikaletwa, wakampakiza Aisha na kuondoka. Ndani ya helkopta, muda wote Mike alikuwa amemuegemeza mpenzi wake katika mapaja yake, kila alipomwangalia, alimuonea huruma na alisikia maumivu makali moyoni mwake.


Helkopta iliondoka na baada ya dakika kumi, Kisiwa cha West Point kikaanza kuonekana machoni mwao. Safari ya kuelekea Marekani ilikuwa ndefu sana na wasingeweza kufanya hivyo kwa kuhisi kwamba Aisha angeweza kufa hata njiani, hivyo kilichofanyika ni kutua katika kisiwa hicho kwa ajili ya matibabu.


Helkopta ilipotua tu, wakamshusha na kumbeba na kumpeleka katika hospitali ambayo haikuwa mbali na mahali hapo helkopta ilipotua. Watu wa kisiwa hicho walibaki wakiwaangalia tu, hawakujua hao walikuwa wakina nani, walitoka wapi na walifuata nini mahali hapo.


“Anaumwa nini?” aliuliza nesi mara baada ya kufika hospitalini hapo.


“Anaumwa njaa, kingine ni kwamba mimba inataka kuharibika...” alijibu Mike, hata Shawn mwenyewe hakuwa na nguvu za kujibu.


Machela ikasukumwa mpaka katika chumba kimoja ambapo huko Aisha akalazwa katika kitanda kimoja, kitu cha kwanza kabisa kufanyika ni kuchomwa sindano ya glucose kwa ajili ya kuupa nguvu mwili wake.


“Dokta, atapona?” aliuliza Mike, kwa kumwangalia tu alionekana kuchanganyikiwa.


“Atapona tu, wala usijali!”


Mike hakutaka kuondoka hospitalini hapo, aliwaagiza wenyeji wa kisiwani hapo, Shawn na wenzake wapelekwe katika hoteli ya gharama, wale na kufanya mambo mengine wakati yeye akiendelea kuwa hospitalini hapo.


Hicho ndicho kilichofanyika, wakaondoka huku yeye akiendelea kubaki pale hospitali, kitu alichokitaka ni kuona mpenzi wake angeishia wapi. Alibaki akimuomba Mungu, hakukuwa na kitu kilichokuwa kikimuumiza kama kuona mpenzi wake akiwa hoi kitandani.


Pale alipokuwa, mapigo ya Aisha yakaanza kupata nguvu ya kudunda, yalikuwa mafanikio makubwa, akasafishwa sehemu zake za siri na kupewa dawa zenye nguvu ya kuua bakteria walioanza kushambulia sehemu hiyo.


Hawakuishia hapo, waliendelea hata kumchunguza kwa ndani zaidi kuona kama kulikuwa na tatizo kubwa, walipoona kwamba hakuna tatizo la kutisha, wakamuwekea dawa nyingine yenye nguvu zaidi.


Siku ya kwanza ikapita huku Aisha akiwa hoi kitandani pale, Mike hakutaka kutoka, aliendelea kubaki chumbani palepale mpaka usiku ulipoingia. Kesho yake, akaamka akiwa kwenye kiti, akasimama na kumsogelea Aisha pale kitandani alipokuwa amelala, akamsogelea, hapohapo Aisha akayafumbua macho yake.


“Umeamka hatimaye!” alisema Mike huku akimwangalia msichana huyo usoni.


Aisha hakuzungumza kitu, aliyafumbua macho yake lakini hakuwa na nguvu zozote za kuongea, akabaki akimwangalia mpenzi wake tu. Kidogo moyo wake ukafarijika, ile furaha ambayo ilipotea ikaanza kurudi upya moyoni mwake.


Baada ya siku tatu, kidogo Aisha alionekana kupata nafuu na hivyo kuendelea na safari ya kuelekea nchini Marekani. Mpaka wanaingia, Aisha alionekana kuwa mwenye furaha mno, hakuamini kwamba mwanzo wa safari ile ndefu hatimaye angefika nchini Marekani, sehemu ambayo kulikuwa na watu wengi duniani walikuwa wakiililia.


Maisha yakaanza upya nchini humo, Aisha hakutakiwa kuonekana, kuwa kwake nchini humo ilikuwa siri kubwa, aliishi na Mike kama mke na mume.


Mimba ya Aisha iliendelea kukua, kila siku Mike alikuwa pembeni yake, kuwa karibu na msichana huyo lilikuwa jambo lililompa furaha sana maishani mwake, hakuamini kama mwisho wa siku naye alikuwa akienda kuitwa baba.


“Daktari amesemaje?” aliuliza Mike.


“Mtoto wa kike!”

“Kweli?”

“Ndiyo!”


“Ataitwa Monica...ninakupenda mpenzi wangu!” alisema Mike huku akitoa tabasamu pana.


Siku zikaendelea kwenda mbele, miezi ikakatika na baada ya mimba kufikisha miezi tisa, Aisha akaanza kujisikia uchungu ambapo akachukuliwa na kupelekwa hospitali.


Mike alipopigiwa simu na kuambiwa kilichokuwa kimetokea, hakuamini, akatoka ofisini kwake, hata kabla dereva wake hajafika, akaingia ndani ya gari na kuondoka kuelekea hospitali. Alitaka kufuatilia kila hatua, alipofika, akachukuliwa na kuambiwa kusubiri nje ya chumba cha leba.


“Hakuna tatizo!” alisema Mike na kutulia mahali hapo, baada ya saa moja, akaanza kusikia sauti ya mtoto akilia, akashindwa kuvumilia, akapiga magoti na kumshukuru Mungu! Hatimaye akafanikiwa kuwa baba.





Maisha mapya yakaanza, Mike alionekana kuwa na furaha kupita kawaida, kila wakati alikuwa na mtoto wake, alimpenda Monica kuliko kitu chochote kile katika maisha yake.

Siku ziliendelea kukatika, hakuwa mtu wa kuwahi ofisini kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, mara kwa mara alipokuwa akiamka, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumchukua mtoto wake kisha kumbeba.

Kazi ya kumhudumia ilikuwa juu yake, hakutaka mpenzi wake, Aisha asumbuke kwa kitu chochote kile. Kutokana na mchanganyiko wa rangi aliokuwa nao, Monica alionekana kuwa mrembo tangu kipindi hicho alichokuwa mdogo.

Marafiki wa Mike kila siku walifika nyumbanii hapo kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya, kwake, ilikuwa ni furaha tele. Aisha alikuwa na afya tele, hakutaka kuwasiliana na wazazi wake, alijaribu kusahau kila kitu kilichopita nchini Kuwait na hakutaka urudi tena huko.

Mpaka mwaka wa kwanza unakatimia, Monica alikuwa na uzuri wa sura yake ulionekana kwa kiasi kikubwa. Mike alikuwa na kazi kubwa ya kumpa maisha mazuri binti yake, huyo ndiye alikuwa mtu pekee aliyemthamini.

“Nitamlinda maisha yangu yote...” alisema Mike huku akiwa amembeba Monica katika bustani ya maua.

MIAKA MITANO BAADAYE

Monica alikuwa msichana mrembo mno, kila alipokwenda, kulikuwa gumzo, alikuuwa na sura nzuri, nusu alikuwa mtu mweusi na nusu alikuwa Mzungu. Maisha yake yalikuwa ya kifahari, kila siku baba yake alikuwa na jukumu kubwa la kumfuata shuleni na kisha kumpeleka nyumbani.

Huyo ndiye alikuwa roho yake, alitamani sana kupata mtoto wa pili na walikubaliana mpaka huyo atakapofikisha umri wa miaka mitano, hivyo wakaanza kufanya jitihada za kumtafuta mtoto wa pili.

Siku moja akiwa ofisini, akapigiwa simu na kupewa taarifa kwamba mpenzi wake, Aisha alikuwa hoi, alikuwa akitokwa na damu sehemu za siri na haikujulikana tatizo lilikuwa nini.

Hakukuwa na muda wa kumsubiri daktari wa familia afike bali alichomwambia mfanyakazi wa ndani ni kumpeleka hospitali na haraka sana kitu hicho kufanyika.

Ofisini hakukukalika tena, alichokifanya ni kuondoka na kwenda katika Hospitali ya St. Paul Medical Care ambapo huko akamkuta Aisha akiwa kitandani.

Muda mwingi alikuwa akilia kwa maumivu makali, Mike akamuuliza juu ya tatizo alilokuwa nalo lakini mwanamke huyo hakujibu chochote kile zaidi ya kuonyesha dalili zote kwamba alikuwa akisikia maumivu mno.

Madaktari waliingia kwa zamu, walimtibu na mwisho wa siku kumwambia tatizo alilokuwa nalo, lilikuwa ni miscarriage, yaani kutoka kwa mimba. Pasipo kujua, kumbe Aisha alikuwa na mimba ila kwa bahati mbaya kabisa, mimba hiyo ilikuwa imeharibika kabisa.

“Unasemaje?” aliuliza Mike.

“Mkeo alikuwa na mimba, ila imeharibika,” alijibu daktari.

Mike akaumia moyoni mwake, hakuamini alichokisikia, alibaki akimwangalia daktari yule mara mbilimbili, alihisi kama alikuwa ndotoni. Alihitaji sana mtoto wa pili lakini tatizo lililotokea, lilikiumiza sana kichwa chake.

“Haiwezekani...”

“Ndiyo hivyo!”

****

Mike alitakiwa kukubaliana na matokeo kwamba mchumba wake alikuwa na mimba na bahati mbaya iliharibika na kutoka, moyo wake ulimuuma sana kwani hakukuwa na kitu alichokuwa akikihitaji katika kipindi hicho kama kumuona mchumba wake akizaa tena.

Alibaki kwenye kiti huku akihuzunika, alishindwa kabisa kuyazuia machozi yake akajikuta akianza kulia mahali hapo. Daktari aliyemfuata na kumpa taarifa ndiye aliyekuwa akimpoza, alijua ni kwa namna gani aliumia moyoni mwake hivyo kumfariji lilikuwa jambo la msingi sana.

Baada ya dakika kadhaa, akanyamaza, akaelekea bafuni na kunawa uso wake kisha kurudi tena kule kwenye korido, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba alicholazwa mchumba wake, alipomuona, machozi yakaanza kutiririka tena mashavuni mwake.

Akamsogelea na kuanza kumwangalia, maumivu aliyokuwa nayo moyoni mwake yakaongezeka maradufu, hakuamini kama ingetokea siku ambayo angekuja kuumia kama siku hiyo hasa mara baada ya kumpata msichana huyo wa maisha yake.

“Aisha mpenzi....kwa nini lakini?” alijikuta akiuliza kwa sauti ndogo huku macho yake yakiwa yametua usoni mwa mpenzi wake.

Aisha alikuwa kimya kitandani pale, Mike hakutaka kuondoka, alibaki palepale huku muda mwingi akitumia kumwangalia mpenzi wake. Hakujali kama kulikuwa na baadhi ya majukumu hayakuwa yakiendelea ofisini kwake, kilichokuwa cha muhimu kwa wakati huo kilikuwa afya ya mpenzi wake tu.

Aisha alikaa hospitalini kwa siku mbili na ndipo alipotoka na kurudishwa nyumbani. Maisha yake yalikuwa na huzuni kubwa, mara kwa mara alikuwa mtu wa kulia tu, mpenzi wake ndiye alikuwa mfariji wake mkubwa, alipolia na kuumia moyoni mwake, mwanaume huyo ndiye alikuwa mfariji wake.

Maisha yaliendelea kama kawaida, ukaribu wao haukupungua, kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo walivyoendelea kupendana kila siku. Baada ya miezi sita kupita, wakaamua kuanza tena harakati za kumtafuta mtoto wa pili.

Usiku na mchana kazi yao ilikuwa hiyohiyo lakini kila baada ya wiki mbili Aisha alipokwenda kupima hospitalini, hakukuwa na dalili zozote za mimba. Hilo liliwaumiza sana lakini hawakujali, juhudi zao ziliendelea kila siku lakini matokeo yalikuwa yaleyale kwamba Aisha hakupata mimba.

Hilo likawatisha sana, wakahisi kwamba kulikuwa na tatizo na hivyo kwenda kumuona daktari wa familia, Dk. Cassie ambaye alipomnguza Aisha kwa vipimo vyake akaonekana kuwa na tatizo.

“Kuna nini?” aliuliza Mike.

“Mkeo ana tatizo...”

“Tatizo gani?” aliuliza Mike huku akionekana kuchanganyikiwa.

Wakati daktari aliposema hivyo, moyo wa Aisha ukapiga paa, hakuamini alichokisikia, kitendo cha daktari yule kusema kwamba alikuwa na tatizo, tayari akakosa amani moyoni mwake, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu huku wakati mwingine akitamani kutoka ndani ya chumba kile ili asimsikie daktari akitoa majibu ya vipimo vile.

“Mkeo hatoweza kuzaa tena,” alisema Dk. Cassie huku hata kwa kumwangalia tu machoni mwake, alionekana kuwaonea huruma.

“Unasemaje?”

“Tumejaribu kumpima, tumegundua kwamba viunga vyake vya uzazi vimeharibika, mkeo alishawahi kupata tatizo lolote la kiafya katika mfumo wake wa uzazi?” aliuliza Dk. Cassie.

“Ndiyo! Miezi sita iliyopita, alipata mimba ila ilitoka kwa bahati mbaya,” alijibu Mike.

“Poleni sana, hilo ndilo tatizo lililosababisha haya yote, mfumo wake wa uzazi umeharibika,” alisema daktari huku akifungua faili lake.

Kilisikika kilio kikubwa kutoka kwa Aisha, hakuamini alichokisikia, alimwangalia daktari mara mbilimbili lakini majibu yake hayakubadilika, yalikuwa yaleyale kwamba hakuwa na uwezo wa kuzaa tena.

Mike ndiye alikuwa mfariji wake, hakutaka kumuacha katika kipindi kigumu kama hicho, alimfariji, matatizo aliyokuwa akipitia, hakutakiwa kutengwa, alitakiwa kutiwa moyo na kufarijiwa kila siku.

Aisha akakosa raha, furaha aliyokuwa nayo ikapotea, mtoto wake, Monica ndiye alikuwa mfariji wake na ndiye alikuwa mtoto pekee aliyekuwa naye. Kila alipomwangalia, alijiona kuwa na kila sababu ya kumpenda kuliko kitu chochote kile.

Hakukuwa na mwingine, huyo ndiye alikuwa wake wa pekee. Siku zilikatika zaidi, kuna wakati Aisha alimwambia mumewe, Mike kwamba kama alikuwa na kiu ya kupata mtoto basi angefanya lolote, hata kutembea na msichana mwingine ili mradi apate kile alichokuwa akikitaka lakini Mike hakukubali kabisa. Kwake, Aisha alikuwa kila kitu.

“Mtoto si tatizo,” alisema Mike.

“Ila nahisi unaumia.”

“Hapana mpenzi! Siumii kabisa, kama mtoto si tunaye? Sasa kuna tatizo gani?’ aliuliza Mike huku akimwangalia mkewe usoni.

Huo ndiyo ulikuwa uamuzi wake, hakutaka kumsaliti mpenzi wake, alitaka kuendelea kuwa naye milele yote. Japokuwa kulikuwa na uwezekano wa kutembea na msichana yeyote kutokana na utajiri aliokuwa nao lakini hakuonekana kuwa tayari kufanya hivyo.

Wakati akiwa kwenye mawazo mengi ndipo kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kabisa. Akakumbuka kwamba kabla ya kupata utajiri aliwahi kutoa mbegu zake ambazo daktari alimwambia kwamba zingepandikizwa katika yai la mwanamke na hatimaye kutengeneza mtoto kwani mume wa mwanamke huyo alihitaji sana mtoto.

Alipokumbuka hilo, akatoa tabasamu pana, moyo wake ulikuwa na uhakika kwamba kile alichokifanya daktari yule kilifanikiwa kwa asilimia mia moja, hivyo ilikuwa ni lazima amtafute daktari yule na kumwambia mahali alipokuwa mtoto wake.

“Ni lazima niende huko hospitali! Kama fedha ninazo, kumtunza mtoto wa damu yangu haitokuwa tatizo kabisa,” alijisemea.

Hakutaka kufanya siri, alichokifanya ni kumwambia mke wake, alimhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, tangu alipokuwa amepigika, alipofuatwa na watu asiowafahamu na kisha kupewa fedha kwa kazi ambayo alitakiwa kuifanya.

“Kwa hiyo ukatoa?” aliuliza Aisha.

“Ndiyo! Nilitoa na hizo fedha ndizo zilibadilisha maisha yangu. Ni lazima niitafute damu yangu,” alijibu Mike.

Alidhamiria kuitafuta damu yake. Alikumbuka vilivyo kwamba kazi hiyo ya upandikizaji wa mbegu ulifanyika katika Hospitali ya Marie Stopes iliyokuwa hapo New York na daktari aliyemfanyia kazi hiyo aliitwa kwa jina la Fabian.

“Ni lazima nimtafute...” alijisemea Mike, hakutaka kuchelewa, alichokifanya, siku hiyohiyo ni kuondoka kuelekea katika hospitali hiyo.

****

Njiani, Mike alikuwa na mawazo tele, kila kitu kilichokuwa kikitokea katika maisha yake kilimhuzunisha mno, aliona kabisa kwamba angepata msongo wa mawazo kwa jinsi alivyochanganyikiwa.

Mawazo yake yalikuwa kwa daktari aliyezichukua mbegu zake na kwenda kuzipandikiza katika yai la uzazi la mwanamke, hakuwa na matokeo lakini aliamini kwamba zoezi lile lilikamilika na hivyo mimba kutungwa na mtoto kuzaliwa.

Hakuchukua muda mwingi, akaegesha gari katika eneo la Hospitali ya Marie Stopes ambapo akateremka na kuanza kuelekea ndani. Jina lake lilikuwa kubwa na alijulikana kutoka na utajiri mkubwa aliokuwa nao hivyo kila alipopita, watu walibaki wakimwangalia na wengine kujipitisha karibu naye na kumsalimia.

Alichotaka muda huo ni kuonana na Dk. Fabian na kumwambia kile kilichomfanya kuwa ndani ya hospitali hiyo siku hiyo. Alikuwa na hamu ya kuambiwa kile alichokuwa akikitaka na ndiyo maana baada ya kukumbuka hilo hakutaka kupoteza muda.

Baada ya kuzungumza na nesi mmoja na kumuelekeza mahali ofisi ya daktari huyo ilipokuwa, akaamua kwenda huko. Hakukuta mtu yeyote hivyo akapiga hodi na kuingia ndani.

Sura yake haikuwa ngeni kwa Dk. Fabian, walibaki wakiangaliana tu. Dk. Fabian alimfahamu mwanaume aliyesimama mbele yake, alikuwa bilionea mkubwa lakini hakukumbuka kama mtu huyo ndiye yule ambaye alitoa mbegu zake na kisha kupandikizwa katika yai la Katty.

“Karibu sana Bwana Mike...” alimkaribisha, Mike akakaa kitini.

Kwanza wakaanza kuzungumza mambo mengine kabisa, katika stori zote, Dk. Fabian alitumia muda wake kumsifia Mike kutokana na uchapakazi aliokuwa nao mpaka kumfanya miongoni mwa mabilionea wakubwa duniani.

Katika kumwambia kile alichokuwa amekifuata mahali hapo, hakuanza moja kwa moja, alianzia mbali kabisa tangu alipokuwa msikini, alimwambia mambo mbalimbali aliyoyapitia, maisha magumu aliyokuwa nayo kabla ya kuwa bilionea mkubwa.

Dk. Fabian uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, kila alichokuwa akiambiwa kilionekana kumfurahisha lakini baada ya Mike kuanza kuzungumzia kile kilichomleta mahali pale, Dk. Fabian akaonekana kushtuka.

“Unakumbuka lakini?” aliuliza Mike.

“Kumbe ni wewe?”

“Ndiyo! Naomba uniambie, mtoto wangu yupo wapi,” alisema Mike huku akimwangalia daktari huyo usoni.

Dk. Fabian hakujibu kitu chochote kile, alikumbuka kwamba mara ya mwisho kuzungumza na mtu huyo alimwambia wazi kwamba mbegu zile aliziuza na kila kitu kilichoendelea siku ile kilikuwa siri kubwa, sasa iweje mtu huyo aje na kumwambia kwamba alihitaji mtoto wake?

“Hapana! Unakumbuka tulichokubaliana?” aliuliza Dk. Fabian.

“Kipi?”

“Kwamba iwe siri!”

“Sawa! Itaendelea kuwa siri, kwani nimemwambia mtu?”

“Hapana! Ila zile mbegu ziliuzwa, unakumbuka?” aliuliza Dk. Fabian.

Kwanza Mike hakutaka kuzungumza kitu, alibaki akimwangalia daktari huyo, hasira zake zikaanza kuonekana waziwazi usoni mwake, alimuona daktari huyo kuwa mpumbavu mkubwa.

“Hivi zile ni mbegu za nani?” aliuliza Mike.

“Zilikuwa zako!”

“Mtoto aliyezaliwa ana vinasaba vya nani?”

“Vyako!”

“Sasa kwa nini mtoto asiwe wangu?”

“Lakini tulikubaliana!”

“Najua! Niambie ni nani mwenye mtoto wangu!” alisema Mike huku akimwangalia daktari huyo kwa macho yaliyojaa chuki.

“Hapana! Hiyo ni siri ya hospitali, na ni siri ya taaluma yangu, siwezi kufanya hivyo,” alijibu daktari huyo, macho yake tu yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikisema.

“Kweli?”

“Ndiyo!”

Mike hakutaka kuzungumza kitu, kadiri alivyomwangalia daktari yule ndivyo alivyokasirika zaidi, alichokifanya ni kuinuka na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulikuwa na hasira kali, japokuwa ni kweli aiziuza mbegu zile kipindi cha nyuma lakini kipindi hicho aliona kama amedhulumiwa haki yake hivyo ilikuwa ni lazima aipate tena.

“Nitajua la kufanya!” alisema Mike na kuingia ndani ya gari lake, alichokifanya ni kuondoka hospitalini hapo huku moyo wake ukiwa umejaa hasira kali.




Dk. Fabian hakuwa na raha kabisa, muda wote alikuwa na mawazo tele, ujio wa Mike ndani ya hospitali ile ulimchanganya mno, hakuelewa ni kitu gani alitakiwa kufanya, hakujua kama alitakiwa kumwambia Dylan juu ya kilichokuwa kimetokea au alitakiwa kukaa kimya.


Alijifikiria, kichwa chake kilisumbuka sana, alijiuliza lipi lilikuwa sahihi lakini mwisho wa siku aliona ni bora kumwambia Dylan ukweli kwamba yule mtu ambaye alimuuzia mbegu, alifika ofisini kwake na kudai watoto wake.


“Ila wote si mabilionea! Watajuana wenyewe,” alisema Dk. Fabian na kisha kuchukua simu yake na kumpigia Dylan.


Simu ilipokelewa na sauti ya Dylan kuanza kusikika kutoka upande wa pili. Iliita na Dk. Fabian kuitikia. Walizungumza kidogo na alipotaka kumgusia kuhusu kile kilichokuwa kimetokea, alisita kufanya hivyo na mpaka anakata simu, hakuwa amemwambia lolote lile.


Moyo wake ulikuwa mzito sana, alijiona kuwa kwenye wakati mgumu mno. Alijitahidi kujisahaulisha lakini ilishindikana kabisa. Hakutaka kuendelea kukaa hospitalini hapo, akaondoka zake na kurudi nyumbani.

Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki moja, akampigia simu mkewe na kumwambia kwamba alichukua likizo hivyo wangeondoka na kuelekea katika Visiwa vya Hawaii kwa ajili ya kula bata tu.


Safari hiyo ikapangwa ifanyike baada ya siku mbili, mkewe akajiandaa vilivyo kumsubiri mumewe ili wazungumze vizuri juu ya safari hiyo kwani naye alitamani kuwa na mumewe, waende sehemu, wakae huko kwa siku kadhaa kwani ni muda mrefu ulikuwa umepita pasipo kufanya kitu hicho.


“Nakuja tupange,” alisema Dk. Fabian na kukata simu.


Hakutaka kubaki ofisini, kwa sababu muda wa kuondoka ulikuwa umefika, akatoka ofisini kwake, akachukua begi lake na kisha kutoka. Akaelekea sehemu ya kuegesha magari na kisha kulifuata gari lake huku tayari ikiwa imetimia saa mbili usiku.


Wakati amefungua gari lake na kutaka kuingia ndani, watu watatu waliovalia mavazi ya kidaktari, yaani mavazi marefu meupe wakamsogelea kule alipokuwa. Alibaki akiwaangalia, aliwafahamu madaktari wote wa hospitali hiyo lakini wale hawakuwa madaktari wa hapo kabisa.


“Nyie ni wakina na...” aliuliza lakini hata kabla hajamaliza kuuliza swali lake, akajikuta akionyeshea bastola ndogo aina ta Revolver na kutakiwa kunyamaza, vinginevyo angekufa.


“Shiiiiiii...” alitoa sauti hiyo mwanaume mmoja.


Walichokifanya ni kuingia naye ndani ya gari hilo na kuanza kuondoka naye huku wakimwambia akae katika kiti kingine. Gari likaendeshwa kwa mwendo wa kawaida tu, lilipita katika barabara kubwa ya St. George na baada ya dakika ishirini likaanza kuingia katika gereji moja kubwa ambapo ndani kulikuwa na wanaume wenye miili iliyojazia kama kumi na mbili, mikononi walishika spana na vifaa vingine vya kutengenezea magari. Aliposhushwa tu, wanaume wote hao wakamuonyeshea sura zilizokuwa na tabasamu pana.


“Karibu sana katika dunia yetu....ngoja nikwambie kwa kifupi tu, ukiwa humu, utasema tu tunachokihitaji kukijua, unaweza kusema kwamba hausemi, ila mwisho wa siku, unajikuta ukiwa umesema,” alisema mwanaume mmoja na kisha kumchukua, wakamuweka kwenye kiti, wakachukua bomba kubwa la kuchomelea magari, jamaa akafyatua kitufe, moto wa gesi ukatoa na kuanza kumsogelea Dk. Fabian katika kiti kile alichokuwa.


“Utakuwa tayari kutuambia tunachotaka kukijua?” aliuliza mwanaume mmoja. Dk. Fabian jasho lilimtoka.


“Ndiyo...ndiyo nitawaambia...” alisema huku akitetemeka mno.


“Sawa. Tulia tuanze kukuuliza maswali yetu,” alisema mwanaume huyo na kuuzima moto ule. Akavuta kiti na kutulia mbele ya Dk. Fabian.


Watu waliokuwa mbele yake hawakuonekana kuwa na masihara hata kidogo, walikuwa wazee wa kazi ambao mara wanapokuwa na uhitaji wa kufahamu kitu fulani kutoka kwako, ilikuwa ni lazima uwape ushirikiano kwani bila kufanya hivyo, hawakuwa na huruma hata kidogo.


Jamaa aliyekaa mbele yake, alikaa kitini huku akimwangalia Dk. Fabian, macho yake tu yalionyesha ni kwa kiasi gani hakuwa na maihara mahali hapo, alimwambia mapema sana kwamba alitaka kuambiwa kila kitu alichotaka kuambiwa kwani pasipo kupata alichokihitaji, ule moto wa gesi ungeishi mwilini mwake.


“Nani alipewa mtoto?” aliuliza mwanaume huyo.


“Mtoto gani?” aliuliza Dk. Fabian, hapohapo mwanaume yule akauwasha moto wa gesi, kwake, swali hilo lilikuwa kama dharau.


“Samahani Bwana mkubwa, sijajua unamzungumzia mtoto yupi,” alisema Dk. Fabian, kwani alijua kwa jinsi moto ulivyowashwa, ungeishia mwilini mwake.


“Nazungumzia zile mbegu za kiume ulizokuwa umepandikiza, mtoto alikwenda kwa nani?” aliuliza mwanaume huyo.


Hapo ndipo Dk. Fabian alipopata jibu juu ya watu wale, walikuwa wanaume ambao walitumwa na Mike Wamteka na awaambie mahali mtoto wake alipokuwa. Alikumbuka vilivyo, hakuwa na mtoto mmoja kama alivyohisi bali mbegu zake zilifanikiwa kuleta watoto wawili.


“Kumbe Mike ndiye ananifanyia hivi?” aliuliza Dk. Fabian.


“Sikiliza, una dakika chache sana za kutuambia mahali mtoto alipo, vinginevyo, utaacha mwili wako hapahapa,” alisema mwanaume yule.


Hakukuwa na utani, si huyo mwanaume aliyekaa mbele yake tu alionekana kuwa siriazi, hata wanaume wengine waliokuwa mahali hapo nao walionekana hivyohivyo kwamba hawakuwa na utani hata chembe.


Walitaka kujibiwa maswali yao, hawakutaka maelezo makubwa ambayo waliamini yasingewasaidia kwa chochote kile. Dk. Fabian akanyamaza, akaanza kuwaza kama lilikuwa jambo sahihi kuwaambia wanaume hao kila kitu, ila alivyoona jinsi hali mbaya iliyokuwa ikiendelea ndani ya gereji ile, hakuwa na jinsi.


“Ni kweli upandikizaji wa mbegu ulikamilika...” alisema Dk. Fabian.


“Baada ya hapo?”

“Mwanamke akajifungua...”

“Mwanamke yupi?”

“Mke wa Bwana Dylan..”

“Huyu bilionea?”


“Ndiyo!”


“Unamaanisha wale watoto wake mapacha, au siyo?”

“Ndiyo haohao.”


Hicho ndicho walichotaka kufahamu. Walichokifanya ni kumpigia simu Mike na kumwambia kila kitu walichoambiwa na daktari yule, walimueleza kwamba upandikizaji wa mbegu zile ulifanikiwa na matokeo yake kulikuwa na watoto mapacha, walipomwambia kwamba mtu aliyewekewa mbegu zile alikuwa mke wa Bwana Dylan, hata naye akashtuka.


“Unasemaje?”


“Hayo ndiyo maelezo tuuliyopewa.”


“Sawa! Endeleeni kumshikilia, ninakuta tupange mipango!”


Simu zikakatwa, upande wa pili, Mike alikuwa na mawazo tele, hakuamini kama kweli watoto wa Bwana Dylan ndiyo walikuwa watoto wake. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kufungua laptop yake, akaunganisha na tovuti ya Google na kisha kuandika ‘Bilionaire Dylan’s Family’. Hapohapo picha za Bwana Dylan na familia yake zikaanza kuonekana kwenye laptop yake.


Aliwaangalia vizuri watoto mapacha aliokuwa nao, kwa mbali walionekana kufanana naye kwa kila kitu, alibaki akishangaa, upandikizaji ule ulimfanya kupata watoto wawili mapacha, hakukuwa na kitu kingine alichokitaka kwa wakati huo zaidi ya watoto wake tu.


Akawasiliana na vijana walewale waliomteka Dk. Fabian na kuwapa kazi nyingine kwamba alitaka kuwaona watoto wake ambao walikuwa wakubwa na walikuwa wakisoma shule ya msingi kipindi hicho.


Hilo halikuwa tatizo, vijana hao walikuwa tayari mua wowote ule hivyo wakahakikisha kwamba kila kitu kinakwenda kama kinavyotakiwa kwenda.


Wakaanza kuwafuatilia, kila siku ilikuwa ni lazima kuwafuatilia shuleni, kitu ambacho kiliwapa wakati mgumu ni kwamba watoto hao walikuwa wakipelekwa na kurudishwa shuleni na baba yao ambaye bila shaka alikuwa na bastola.


Hawakutaka kukata tamaa, walimwambia wazi Mike kwamba kazi ilikuwa kubwa sana kwani walihisi kwamba bilionea huyo alikuwa na bastola kitu ambacho kingeweza kuhatarisha maisha yao, pia hawakutaka kufanya hivyo kwani kama angeanza kurushiana nao risasi, ingewezekana kabisa kukosea na hivyo kuwapiga watoto hao.


Hoja zao zikaeleweka kwa Mike lakini akawataka waendelee kufuatilia zaidi pasipo kumuachia huru Dk. Fabian kwani walijua kwamba kama wangemuachia huru basi angekwenda kusema kila kitu kilichokuwa kimetokea.


Baada ya wiki moja tangu walipoanza kufuatilia ndipo wakafanikiwa kugundua kwamba siku hiyo watoto walipokuwa wakipelekwa shuleni, hawakuwa wakiendeshwa na baba yao bali alikuwepo dereva.


Hiyo ikawafurahisha, walichokifanya ni kuvuta subira kwa kuona kwamba pia ua ilikuwa ni lazima wakamilishe mpango wao wakati wa kutoka shuleni, hivyo wakavumilia.


Pembeni ya shule waliyokuwa wakisoma Patrick na Patricia kulikuwa na mgahawa wa McDonald hivyo wakaelekea hapo na kuanza kunywa kahawa huku macho yao yakiwa katika geti la shule hiyo kubwa.


Nje, katika sehemu ya kuegeshea magari waliweza kuliona gari la Bwana Dylan likianza kuingia mahali hapo, wakaangalia ndani, hakuwepo zaidi ya dereva tu aliyefika mahali hapo kwa ajili ya kuwachukua.


Hawakutaka kuchelewa, nao wakatoka katika mgahawa ule na moja kwa moja kuanza kulifuata. Bastola zilikuwa mikoni mwao, siku hiyo ilikuwa ni lazima wakamilishe kile walichokuwa wakikihitaji, wawateke watoto hao na kisha kuondoka nao.

Walipolifikia gari hilo, jamaa mmoja akakifuata kioo na kuanza kukigonga huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana ambalo lilimfanya dereva kutokugundua kama mtu huyo alikuwa mbaya, tena alikuwa na wenzake waliojificha. Akashusha kioo.


“Nikusaidie nini kaka?” aliuliza dereva huku akimwangalia mtu huyo.


“Hakuna chochote, ninataka tu utulie hivyohivyo!”

“Kwa nini?”


Mwanaume huyo hakuzungumza kitu kingine chochote kile zaidi ya kutoa bastola yake na kumnyooshea dereva huyo ambaye akaanza kuogopa kwani tangu azaliwe, hakuwahi kuonyeshewa bastola hata mara moja.


“Kaka, gari siyo yangu! Ni ya bosi wangu,” alijitetea.


“Hatuhitaji gari...”

“Hamuhitaji?”


Hapohapo wenzake wakajitokeza, wote walikuwa na bunduki, wakafungua milango na kuingia ndani huku wakimtaka dereva huyo atulie hivyohivyo na hata watoto hao watakapokuja, awatambulishe kwamba wao walikuwa marafiki zake. Dereva akatii kwani pasipo kufanya hivyo, aliamini angeweza kuuawa.




Kama kawaida yao, Patrick na Patricia walitoka darasani na kuanza kuelekea katika sehemu ya kupakia magari ndani ya eneo hilo kwa ajili ya kuingia ndani ya gari lao na kisha kuondoka mahali hapo. Walikuwa wakirukaruka, hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya kila walipoachwa watembee pamoja.


Walikuwa wamependeza mno, walivutia, kufanana kwao ilikuwa vigumu mno kugundua yupi alikuwa mwanaume na yupi mwanamke kwani hata Patricia mwenye hakutaka kuachia nywele ndefu, zilikuwa fupifupi kama zilivyokuwa za ndugu yake.


Mara baada ya kulifikia gari lile, mlango ukafunguliwa na kisha kuingia ndani. Kwanza wakashtuka, hawakumkuta dereva peke yake kama ilivyokuwa asubuhi, walimkuta akiwa na wanaume wengine watatu, ingawa sura zao zilionyesha tabasamu pana lakini hawakutaka kuamini kama watu wale walikuwa wazuri.


“Kaka, ni wakina nani hawa?” aliuliza Partick huku akimwangalia mtu mmojammoja ndani ya gari hilo.


“Ni marafiki wa baba, twendeni,” alisema dereva yule.


Hawakubisha, wakaingia ndani na kisha safari ya kuelekea nyumbani kuanza. Walionekana kuwa na hofu, hawakuonekana kujiamini hata kidogo, kila walipowaangalia watu hao, walizidi kuogopa na kuona kwamba watu hao hawakuwa marafiki hata kidogo.

Hawakuchukua barabara ile waliyozoea ya kurudia nyumbani, wakachukua barabara nyingine, na sehemu zote walizokuwa wakipita, dereva ndiye aliyekuwa akiambiwa nenda huku, kata huku, nenda kule.


“Tunakwenda wapi?” aliuliza Patricia huku akionekana kuwa na wasiwasi.


“Nyumbani!” alijibu dereva kwa kifupi.


“Hapana! Ila huku siyo nyumbani, kaka turudishe nyumbani,” alisema Patricia huku hofu yake ikionekana dhahiri machoni mwake.


Dereva hakuwa na la kufanya, alikuwa akiambiwa nini cha kufanya na wapi pa kupita, walipofika umbali fulani, wakamwambia atoke katika kile kiti na jamaa mmoja kukalia.


Hawakutaka kumuacha hapo, walijua kwamba kama wangefanya hivyo basi ingekuwa ni rahisi kutoa taarifa kituo cha polisi, wakaondoka naye, walipofika katika ile gereji ambayo ndani yake bado walimshikilia Dk. Fabian, wakamuingiza na dereva huyo na kumwambia atulie na wao kuendelea na safari yao.


Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Patrick na Patricia walikuwa wakikifuatilia kwa karibu mno, walikuwa wakilia tu, walitaka kurudishwa nyumbani lakini hakukuwa na mtu aliyewasikiliza zaidi ya kuambiwa kwamba huko walipokuwa wakipelekwa ndipo palikuwa kwa baba yao.


“Tunataka kumuona mama, turudisheni nyumbani, tunataka kumuona mama...” alisema Patricia huku akilia mfululizo, si yeye tu, hata Patrick naye alikuwa akilia tu.


“Nyamazeni, huku tunapokwenda ndipo kwa baba yenu,” alisema jamaa mmoja.


Hawakunyamaza, kilio chao kilikuwa hichohicho lakini hakukuwa na aliyewaelewa, baada ya dakika kadhaa, gari hilo likaanza kuingizwa katika jumba moja kubwa, lilikuwa ni zaidi ya nyumba waliyokuwa wakiishi, kulikuwa na bwawa la kuogelea, walinzi, mbwa na vitu vingine vingi.


Baada ya gari kutembea kwa umbali fulani ndani ya eneo kubwa la nyumba hiyo, likasimamishwa na kisha kuteremshwa kutoka ndani ya gari hilo. Walikuwa kwenye hofu, wakachukuliwa na kuingizwa ndani, wakaambiwa wakae kwenye makochi yaliyokuwa hapo sebuleni.


Baada ya dakika kadhaa, Mike akatokea sebuleni hapo, alikuwa na mpenzi wake, Aisha. Alipowaona watoto hao, akashindwa kuvumilia, alifanana nao sana, akawasogelea na kisha kuwakumbatia.


Walimwangalia mwanaume huyo, hawakumfahamu alikuwa nani, ndiyo kwanza ilikuwa mara yao ya kwanza kumuona. Aisha alisimama pembeni, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, alipowaangalia watoto hao, alikuwa na uhakika walikuwa watoto wa mpenzi wake kwani kama kufanana, walifanana naye sana.


“Watoto wangu! Hatimaye mpo mikononi mwangu,” alisema Mike huku akiwaangalia, bado Patrick na Patricia walionekana kuwa na wasiwasi.


“Tunataka kwenda nyumbani!”


“Hapa ndiyo nyumbani kwenu!”


“Hapana! Tunataka kumuona mama na baba...” alisema Patricia.


“Mimi ndiye baba yenu! Patricia, mimi ni baba yako, niangalie, huoni kama tunafanana?” alisema Mike huku akimwangalia Patricia usoni, hakuishia hapo, maneno hayohayo akamwambia na Patrick.


Ni kweli, walipokuwa wakimwangalia mwanaume huyo aliyesimama mbele yao walifanana naye sana lakini hiyo haikutosha kumaanisha kwamba alikuwa baba yao, walifahamu fika kwamba Dylan ndiye alikuwa baba yao, sasa kwa nini mwanaume huyo aseme kwamba alikuwa baba yao, kwao, hilo lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo.


****


Bado Dylan na mkewe walikuwa kwenye mawazo lukuki, kitendo cha watoto wao kutokuonekana kiliwachanganya sana, walikuwa kwenye majonzi makubwa, walijitahidi kuwasiliana na polisi lakini hao wala hawakusaidia kitu chochote kile, bado mbele yao kulikuwa na giza nene, hawakujua watoto hao walikuwa mahali gani.


Polisi chini ya Interpool walihangaika lakini hawakufanikiwa, walijaribu hata kuwasiliana na polisi wa nchi nyingine za jirani kama Canada na Mexico ili kuona kama watoto hao watakuwa wamepelekwa huko lakini majibu yalikuwa bila kwa bila.


Hawakutulia, waliposhindwa kabisa, wakawaachia maofisa wa FBI wafuatilie ili kuona kama wangeweza kufanikiwa, wakaingia katika kazi ya kuwatafuta watoto hao, walitakiwa kufanya juu chini lakini mwisho wa siku watoto hao wanapatikana, tena wakiwa salama kabisa.


“Mtu wa kwanza atafutwe dereva, huyu ndiye atakuwa mtu muhimu sana,” alisema afisa mmoja.


Hicho ndicho walichotaka kukifanya, mtu wa kwanza ambaye alitakiwa kupatikana kwa wakati huo alikuwa huyo dereva, naye, kupatikana kwake ilikuwa ngumu sana kitu kilichowafanya maofisa wa FBI kuchukua namba yake ya simu kutoka kwa Dylan ili waweze kuitraki namba hiyo na wafahamu mahali alipokuwa.


“Kama tukifanya hivyo, tutafanikiwa,” alisema afisa wa FBI na kisha kuondoka kuelekea nyumbani kwa Dylan huku wakiwa na uhakika kwamba watafanikiwa kumpata dereva huyo kabla ya kumpata mtu aliyewateka watoto hao.


****


Mara baada ya kuondoka kuelekea nyumbani kwa Dylan, wakaonana naye na kumwambia mikakati kabambe ambayo walitaka kuifanya kipindi hicho, ilikuwa ni lazima waitraki simu ya dereva huyo kujua alikuwa mahali gani kipindi hicho.


Wakapewa namba na moja kwa moja kurudi makao makuu. Huko, wakakaa chini. Suala la kutekwa kwa watoto wa Dylan lilikuwa kubwa, Marekani ikaonekana kama kutikisika kwani Dylan hakuwa mtu mdogo, alikuwa bilionea mkubwa hivyo suala lake lilichukuliwa na kuwa kubwa mno.


Wakaanza kazi mara moja, ilikuwa ni lazima wakamilishe mchakato wao. Vijana wa IT wakakaa katika kompyuta zao, walikuwa ni vijana wenye uwezo ambao waliajiriwa kwa ajili ya kazi hiyo tu.

Walikuwa na PhD ya masuala ya kompyuta, hawakuwa watu wa mchezo hata mara moja. Wakati wao wakihangaika kuitafuta simu hiyo, maofisa wengine wa FBI walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.


“Simu inaita...” alisema kijana mmoja.


Hapohapo wakaingiza katika system yao, ilikuwa ni afadhali simu kuzimwa kuliko kuwa hewani, kitendo cha kuita tu, tayari mambo yakaanza kwenda sawa katika kompyuta zao.


Kwanza ikatokea dunia, ikaanza kujizungusha, ilipofika katika Bara la Marekani ya Kaskazini, ikatulia na hapohapo kuanza kujivuta mpaka katika Jiji la New York, bado ilikuwa ikitafuta mahali simu hiyo ilipokuwa, ikaanza kupita katika mitaa mingi na mwisho wa siku kusimama katika gereji moja iliyokuwa katika Mtaa wa Hampishire ambao ulikaliwa na Waingereza wengi.


“Yupo hapa,” alisema kijana mmoja, mshale ulisimama katika gereji hiyo.


Hapohapo simu zikaanza kupigwa, maofisa wa FBI wakawasiliana na wenzao ambao waliwataka kwenda katika gereji hiyo mara moja, hakukuwa na uda wa kupoteza, haraka sana wakaanza kwenda huko, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, taarifa ilikuwa ikitolewa.


****


Dereva alihisi simu yake ikiita mfukoni mwake, ilikuwa katika mtetemo (vibration) kiasi kwamba hakukuwa na mtu mwingine aliyeligundua hilo. Hakuweza kuipokea, mikono yake ilifungwa kamba na aliiacha iendelee kuita huku akihisi kwamba mpiga alikuwa bosi wake, Dylan.


Hakujua nani mwingine alikuwa mahali hapo, uso wake ulifunikwa kwa kitambaa cheusi, hakuwa akiona kitu chochote kile, hata yule Dk. Fabian ambaye naye alifungwa kamba hakujua kama aliendelea kuwa mahali hapo au alitolewa.


Aliwasikia watu wakizungumza, mazungumzo yao mengi yalikuwa ni kuhusu malipo ambayo walipewa, yalikuwa makubwa ambayo hawakudhani kama kuna siku kungetokea mtu ambaye angewalipa kiasi kikubwa cha fedha kama walicholipwa kwa kufanya kazi nyepesi kama ile ambayo waliifuatilia kwa kipindi cha mwezi mzima.


Mpaka kufikia hatua hiyo, dereva akabaki akijiuliza maswali mengi, hao watu walikuwa nani na kwa nini waliwateka watoto? Hakujua. Muda ulizidi kwenda mbele, hofu yake iliendelea kuwa moyoni mwake na kuna kipindi alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yake.


“Jamani...mnataka nini kutoka kwetu?” aliuliza dereva yule huku akitaka kufahamu kile hasa kilichomfanya kuwa hapo kwani kama suala lilikuwa ni watoto, walichukuliwa na kupelekwa sehemu.


“Wewe! Hebu nyamaza, tutasambaratisha ubongo wako,” alijibu mwanaume mmoja huku akimsogelea, alipomfikia, akampiga teke la uso.


Ilipofika saa kumi jioni, mara honi zikaanza kusikika kutoka nje ya gereji hiyo, walipotazama kupitia kamera zilizokuwa humo ndani, macho yao yakatua katika gari moja la kifahari ambalo lilionekana kubondeka mbele.


Dereva wa gari hilo alikuwa akipiga honi, alitaka kufunguliwa kwa ajili ya kuliingiza gari lake ndani na kufanyiwa matengenezo. Kila mmoja alionekana kukasirika, hawakutegemea kupata gari lolote lile japokuwa hiyo ilikuwa ni gereji.


“Ni nani huyo?” aliuliza jamaa mmoja.


“Sijui! Hebu kamfungulie usikie anataka nini,” alisema jamaa mwingine.


Jamaa huyo akatoka na kuelekea nje ambapo akalifungua geti kwa kuelekea juu, akalifuata gari hilo na kuanza kuzungumza na dereva. Hakutaka kusikia chochote zaidi ya kumwambia kwamba hakuna huduma yoyote iliyokuwa ikitolewa kwa siku hiyo.


Wakati akiwa anazungumza na dereva huyo, wenzake walikuwa ndani wakifuatilia, walitaka kufahamu kama mtu huyo kweli alihitaji kutengenezewa gari au kulikuwa na jingine.


“Sikiliza...” alisema mwanaume aliyekuwa ndani ya gari pamoja na mwenzake.


“Kuna nini tena?”

“Unaliona gari hilo hapo mbele...”


“Limefanyaje?”

“Linahitaji matengenezo.”

“Sawa! Ila gereji imefungwa.”

“Inafungwaje na wakati nilitoa taarifa kwamba nitaleta gari langu?” aliuliza mwanaume huyo, alionekana kumfahamu mtu aliyehusika na gereji hiyo.


“Tumefunga.”

“Kwani wewe ni nani?”

“Mhusika wa hii gereji!”

“Acha ujinga, tangu lini ukawa mhusika wa gereji hii?” aliuliza mwanaume huyo huku akiteremka kutoka ndani ya gari.


Mwenzake hakubaki, naye akatoka, wale vijana wawili waliokuwa ndani ya gereji hiyo ambao walikuwa wakifuatilia kila kitu kwenye televisheni iliyounganishwa na kamera za CCTV, nao wakatoka na kwenda kule nje kwani walihisi kulikuwa na kitu kibaya.


“Kuna nini tena?” aliuliza mwanaume mmoja ambaye ndiye alionekana kuwa kiongozi.


“Nataka kuingiza gari ndani!”


“Ili?”

“Litengenezwe, huoni lilivyo?” alijibu.


“Tumefunga.”

“Kwani nyie ni nani? Mbona hamjakaa kiufundi?” aliuliza.


Wakati mwanaume huyo akijiandaa kujibu, akajikuta akiwekwa chini ya ulinzi na mwanaume yule aliyekuwa upande wa pili. Wenyewe walishtuka, hawakujua hao walikuwa wakina nani, walichokifahamu ni kwamba walikuwa wateja ambao walifika kwa ajili ya kulitengeneza gari lao bovu, sasa iweje wawaweke chini ya ulinzi.


Hawakuwa na jinsi, wakatakiwa kulala chini tena kifudifudi na mikono ikiwa kichwani. Wwalishindwa kufahamu hao walikuwa wakina nani lakini baada ya kutamka kwamba walikuwa FBI, tayari wakajiona kukamatwa.


Wakafungwa pingu na kisha kutulizwa pembeni, kilichofanyika ni kuingia ndani na kisha kuwatoa vitambaa mateka hao ambao ni Dk. Fabian na dereva wa Dylan, kilichofuata ni kupigwa simu makao makuu ambapo baada ya muda, polisi wakafika na kisha kuwachukua na kuwapeleka kituoni.


“Tuambieni watoto wapo wapi?” waliulizwa wanaume hao.


“Hawakuwa pale, walichukuliwa na baba yao,” alijibu mwanaume mmoja.


“Baba yao?”

“Ndiyo!”


Wakaweka wazi kwamba wao walipewa kazi ya kuwateka watoto hao kwa kuwa baba yao alikuwa akiwahitaji, sisi hatukuwa na jinsi, tuliangalia zaidi pesa hivyo kufanya kazi yetu, walipomleta dereva, wakaondoka na watoto hao na kusema wanawapeleka kwa baba yao.


Ofisa wa FBI hakutaka kuuliza swali jingine, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia Dylan huku akimtaka mahali hapo kwani tayari dereva alipatikana, mbali na huyo, pia kulikuwa na wanaume wengine ambao ndiyo waliowateka watoto wao, nao walipatikana.


Ndani ya dakika kumi, Dylan, mkewe na Catherine wakafika mahali hapo. Kwa kumwangalia Dylan alionekana kuwa na hasira mno. Akataka kupelekwa ndani ya chumba hicho.


“Subiri kwanza...tumewauliza wale jamaa, wamesema kwamba watoto unao wewe...” alisema afisa wa FBI.


“Mimi?”

“Ndiyo!”

“Hebu nionane nao,” alisema Dylan.





Kwa jinsi alivyokuwa, haikuwa rahisi kumkubalia, alionekana kuwa na hasira sana hivyo kuona kwamba kama wangemruhusu kuingia ndani basi angeweza kuanzisha timbwili huko ndani.


Wakati hayo yote yakiendelea, Dk. Fabian alikuwa katika chumba kingine na dereva, walikuwa wakizungumza lakini muda mwingi daktari huyo alionekana kuwa na mawazo tele.


Kitu kilichompa mawazo ni kuhusu Mike ambaye aliibuka tena na kuhitaji watoto wake. Alimfahamu kama bilionea lakini alisahau kwamba huyo mwanaume ndiye yule aliyemfuata kipindi cha nyuma na kumtoa mbegu zake za kiume.


Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia Dylan na mkewe, mwanamke hakujua kitu chochote kile kwani mchezo mzima ulipangwa na wao watatu tu. Alijua kwamba mwanaume huyo angeumia sana lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima amwambie ukweli kilichokuwa kimetokea.


Maofisa wa FBI walisubiri kwa dakika arobaini na tano, wakamchukua Dylan na kumpeleka katika chumba walichokuwa mwanaume yule, walitaka kuzungumza nao na kuwauliza kuhusu mahali watoto walipolekwa, walisema walichukuliwa na kupelekwa kwa baba yao, mbona baba mwenyewe alisema kwamba hakuwa amewapata watoto hao?


“Ulisema kwamba watoto walipelekwa kwa baba yao, si ndiyo?” aliuliza afisa wa FBI, pembeni yake akiwepo Dylan na mkewe, Katty.


“Ndiyo!”


“Wazazi wao ndiyo hawa hapa, mbona wanasema hawakuwapata watoto wao?’ aliuliza afisa yule huku akiwaangalia.


“Mkuu! Ila sisi tuliambiwa kwamba wanapelekwa kwa baba yao!”


“Sasa mbona hajawapata? Baba yupi?”


“Baba yao!”


“Si ndiye huyu! Mbona hajawapata?”


“Hata sisi hatujui!”


Walichokifanya FBI ni kumchukua Dk. Fabian na kisha kuwapeleka katika chumba kingine cha mahojiano, huko walitaka kufahamu sababu za wao kutekwa kwa kuhisi kwamba kupitia wao wangeweza kupata kitu fulani.


Alipoulizwa dereva, alisema tu kwamba alikwenda kuwachukua watoto hao, ghafla akatekwa yeye na watoto na kupelekwa gereji, watoto wakachukuliwa na kupelekwa kwa baba yao, kitu ambacho aliona si kweli.


“Na wewe dokta?” aliuliza afisa, Dk. Fabian akakaa kimya, maofisa wote waliokuwa humo ndani wakabaki wakimwangalia, hawakujua sababu ya kukaa kimya, alipomaliza kuwa katika hali hiyo, akauinua uso wake na kuwaangalia.


“Naomba nionane na BwanaDylan!” aliwaambia maofisa wale.


Hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa alimhitaji huyo, afisa mmoja akatoka na kwenda kumuita, baada ya dakika moja tu, akarudi akiwa na Bwana Dylan ambaye alikuwa akiongozana na mkewe.


“Naomba tupewe chumba cha siri, tuna mazungumzo binafsi...” alisema Dk. Fabian, hata Bwana Dylan akabaki akishangaa, kwanza kitendo cha kumuona daktari huyo hapo polisi, kilimchanganya.


Wakapelekwa katika chumba kimoja cha siri, hakukuwa na kamera za CCTV wala hakukuwa na vinasa sauti. Huko wakatulia, muda wote Bwana Dylan alikuwa akimwangalia daktari yule, alihisi kulikuwa na kitu.


“Kuna nini?” aliuliza.


“Mike amerudi!”


“Mike! Ndiye nani?”


“Yule bilionea!”


“Unamzungumza huyu Mike bilionea, amerudi kutoka wapi sasa?” aliuliza Bwana Dylan.


“Unakumbuka zile mbegu tulizozitoa, zilikuwa zake na ndiye yeye aliniteka na kuniuliza nilimuwekea nani mbegu zile, nilikataa kusema, akatishia kuniua..” alijibu Dk. Fabian na kuhadithia kila kitu kilichotokea.


Bwana Dylan alibaki kimya, mwili ulikuwa ukimtetemeka, japokuwa ndani ya chumba kile kulikuwa na kiyoyozi lakini alihisi kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini alichokisikia kwamba yule Mike ambaye alifanikisha zoezi zima la upatikanaji wa watoto wale eti alirudi na kuwataka watoto wake.


“Haiwezekani! Nilimalizana naye, wale ni watoto wangu na si wake ni wangu,” alisema Dylan huku akionekana kuchanganyikiwa.


Hali ya hewa ilibadilika, wakatoka ndani ya kile chumba, kwa jinsi alivyokuwa Dylan kipindi kifupi kilichopita, alionekana kuwa tofauti kabisa na kipindi hiki. Alionekana kuwa mwingi wa hasira, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile.


“Kuna nini?” aliuliza afisa mkuu wa FBI, Bwana Pierre August.


“Nataka nizungumze na wewe...” alijibu Dk. Fabian.


“Kuhusu nini?”


“Aliyewateka watoto.”


“Unamjua?”


“Ndiyo!”


“Ni nani?”


“Bilionea Mike...”


“Unasemaje?”


“Ndiyo hivyo! Ila kuna kitu....”


“Kitu gani?”


“Mtafuteni yeye kwanza...” alisema Dk. Fabian.


Maofisa wa FBI hawakutaka kusubiri, waliambiwa juu ya mtuu aliyekuwa amewateka watoto hao, alikuwwa bilionea mkubwa, hawakujua sababu ya kuwateka hivyo walichokifanya ni kuanza kwenda nyumbani kwake.


Huku nyuma, Dylan alikuwa amechanganyikiwa, akaona kama dunia ikiimgeuka, hakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna ile, alimwangalia mke wake, alionekana kuwa mtu mwenye maswali mengi lakini hakutaka kuzungumza kitu chochote kile.


Kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa siri kubwa na muda huo ulionyesha kabisa kwamba ile siri iliyodumu kwa miaka yote ilikuwa ikienda kujulikana, angefanya nini? Hakujua.


Polisi na maofisa wa FBI wakaelekea mpaka nyumbani kwa Mike, wakaoba kuonana naye, wakaruhusiwa kuingia ndani. Walipofika sebuleni, macho yao yakatua kwa watoto waliokuwa wakiwatafuta, walionekana kuwa kawaida, hawakuwa na furaha wala hawakuwa na huzuni.


Mike alikuwa sebuleni hapo pamoja na mkewe, Aisha, walikuwa wakizungumza mambo mengi na watoto wale, kwa kutumia maneno mengi, bado Mike alikuwa akiwaambia kwamba yeye alikuwa baba yao.


“Na mama yetu ni nani?” aliuliza Patrick.


“Huyo aliyewazaa...”


“Nini kilitokea?” aliuliza Patricia.


“Ni stori ndefu sana, ila nataka mfahamu kwamba mimi ndiye baba yenu,” alisema Mike.


Maofisa hao waliposimama kwa muda, waliimwangalia Mike na mkewe, hawakuonekana kuhofia kitu chochote kile, walichokifanya, hapohapo wakamwambia juu ya kile kilichotokea kwamba alikuwa akishutumiwa kuwateka watoto.


“Sikuwateka watoto...” alijibu Mike.


“Kumbe wamefikaje hapa?”


“Nilikwenda kuwachukua, hivi kweli kuna mtu anaweza kuwateka watoto wake?” aliuliza Mike huku akiwaangalia maofisa hao.


“Watoto wako hawa?”


“Ndiyo!”


Kila mmoja alionekana kumshangaa, walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka katika kituo cha polisi huku akiongozana na mapacha wale. Mike hakuonekana kuogopa hata mara moja, njia nzima uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.


Walipofika katika kituo hicho, wakaingizwa ndani ambapo huko wakakutana na Bwana Dylan akiwa na mkewe, Katty. Patrick na Patricia walipomuona mama yao, wakamfuata na kumkumbatia, walionekana kuwa na furaha mno.


“Mlikuwa wapi?” aliuliza mwanamke huyo.


“Tulikuwa kwa baba...”


“Baba gani?”


“Baba yetu....”


“Yupi?”


“Huyu hapa!” walijibu huku wakimnyooshea mkono Mike.


Hakukuwa na kitu kilichomuuma Dylan kama kuona watoto wake wakimtaja mwanaume mwingine kwamba ndiye baba yao. Aliyasikia maumivu makali moyoni mwake, yaani kitendo cha Mike kukaa na watoto hao kwa muda mfupi tu tayari aliwaambia maneno mengi, kuwashawishi kwa mifano mpaka watoto wote kuamini kwamba yeye alikuwa baba yao.


Dylan hakujibu kitu, alikwenda pembeni na kutulia kwenye kiti. Muda wote machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea mahali pale.


Katty alibaki na maswali mengi, alipomwangalia Mike, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana lakini alipoyapeleka macho kwa mumewe, alikuwa akilia kwa uchungu, hakujua kitu gani kilitokea, katika kumbukumbu zake, hakukumbuka kama alikwishawahi kuonana na Mike, sasa iweje hao watoto wawe wake? Kila alichojiuliza, akakosa jibu.


“Wewe unasema watoto hawa ni wako! Si ndiyo?” alisema Bwana August huku akimwangalia Mike.


“Ndiyo!”


“Kivipi?”


“Dylan anaelewa kila kitu! Watoto ni wangu! Hii ni damu yangu!” alijibu Mike huku akionekana kujiamini.


“Unanichanganya!”


“Angalia hata sura zetu, huoni kama nafanana nao sana...”


“Hilo si tatizo!”


“Basi muulize Dylan, hawa ni watoto wa nani!” alisema Mike.


Bwana August akamgeukia Dylan ambaye alikuwa pembeni akilia tu. Kila mmoja alimuonea huruma lakini ilikuwa ni lazima ukweli ujulikane kwamba hao watoto walikuwa wa nani.


Mke wake mwenyewe alibaki akimwangalia, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Bado alichanganyikiwa, kwa nini mumewe ajiumeume na wakati alijua fika kwamba watoto wale alizaa nao. Kila Dylan alipoulizwa, alibaki kimya.


“Hawa ni watoto wangu! Dk. Fabian, hebu eleza kila kitu kilivyokuwa!” alisema Mike huku bado tabasamu lake likionekana kuwa usoni mwake.


Ilikuwa ni lazima ukweli ujulikane, hata Catherine, mdogo wake Dylan alibaki kimya akiangalia kilichokuwa kikiendelea. Yeye mwenye alichanganyikiwa, kila alipowaangalia mapacha wale, walifanana mno na Mike ambaye alidai kwamba ndiye alikuwa baba wa watoto wale.


Hapo ndipo Dk. Fabian alipoanza kusimulia, alitakiwa kufanya hivyo, hakutakiwa kunyamaza au kuficha kitu chochote kile, alitakiwa kuzungumza ukweli juu ya kila kitu kilichotokea huko nyuma.


Kila mtu alibaki kimya akimsikiliza, muda wote huo, Dylan alijiinamia, machozi mfululizo yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake. Alikuwa tajiri mkubwa, aliyeheshimika, hapo ndipo akagundua kwamba utajiri haukuwa na maana yoyote ile.


Ulikuwa na uwezo wa kununua dawa ila si uhai, ulikuwa na uwezo wa kununua magari ila si furaha. Maneno aliyokuwa akizungumza Dk. Fabian yalimuumiza mno, kila alipoyasikiliza, alihisi kuna mtu alichukua mkuki wenye ncha kali iliyounguzwa na moto na kisha kuuchoma moyo wake.


Mpaka anamaliza kusimulia, Katty alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kimesimuliwa. Yaani kila siku alijua kwamba watoto wale walikuwa wake na mume wake kumbe nyuma ya pazia kulikuwa na kitu kingine, kumbe alipandikiziwa mbegu katika mfumo wake wa uzazi.


Kilio kilisikika kwa sauti ya juu, hakukubali hata mara moja, akamfuata mumewe na kuanza kumgombeza huku akilia, moyo wake ulijisikia uchungu, kama mumewe alikuwa na tatizo, kwa nini hakumwambia kabla. Kila siku alikuwa akifanya naye mapenzi, alikuwa akifanya na nini? Kila alipojiuliza, alichanganyikiwa.


Dylan hakuzungumza kitu, hakutaka kubaki mahali hapo, akatoka nje na kuanza kuondoka huku dada yake akiwa nyuma akimfuata.


“Dylan, unakwenda wapi?” aliuliza Catherine, tayari Dylan alikuwa ndani ya gari, naye akaingia.


“Catherine, nitaishi vipi? Nitaificha wapi sura yangu?” aliuliza Dylan, alikuwa akiendelea kulia tu.


“Unakwenda wapi? Nijibu!”


“Niache, sioni umuhimu wa kuishi, sioni umuhimu wa kuwa tajiri. Nimeumia, utajiri hauna maana, ni utajiri wenye uchungu, utaniliza kila siku. Kwa nini? Kwani imekuwa hivi? Kwa nini Catherine?” aliuliza Dylan, alikuwa akilia mno, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno.


Catherine mwenye hakujibu maswali hayo, alibaki akimwangalia kaka yake, kwa jinsi alivyoonekana tu, alikuwa na maumivu makali moyoni mwake, hakujua nini cha kumwambia na hakutaka kumuache kaka yake kwani alijua ni kitu gani kingetokea endapo angemuacha, ilikuwa ni lazima ajiue kwani alikata tamaa, hakuona umuhimu wa kuishi.


Akawapigia simu wazazi wake, akawaelezea kwamba anahitaji msaada mkubwa kutoka kwao kwani vinginevyo Dylan angejiua. Wazazi wao walichanganyikiwa kusikia hivyo, wakaahidiana waonane nyumbani kwa Dylan.


“Naomba niendeshe gari tafadhali,” alisema Catherine, Dylan akampisha, akashikilia usukani na kuanza kuondoka.


Huku ndani, Katty hakujua afanye nini, alibaki kimya huku akiwaangalia watoto wake, kila alichokisikia hakukiamini, alimchukua mumewe, Dylan kwa kile alichomfanyia, uamuzi wa kuondoka mahali hapo na watoto wake ndiyo uliomjia kichwani, hakutaka kurudi nyumbani, alipanga kuondoka haraka sana kuelekea Los Angeles.


“Katty...samahani sana kwa kilichotokea, hakikuwa dhumuni langu, najua umeumia sana lakini haina jinsi, naomba unisamehe kwa kila kitu,” alisema Mike huku akimwangalia mwanamke huyo.


“Usijali...”


“Sasa unakwenda wapi?”


“Ni lazima niende Los Angeles, siwezi kubaki hapa...”


“Na watoto wangu?”


“Ni watoto wangu pia...”


“Najua! Lakini ningependa kuwa nao karibu!”


“Najua!”


“Kwa hiyo tufanye nini?”


Moyoni mwake aliumia, kila kitu alichokiacha nyumbani, hakutaka kukirudia, aliamua kuondoka kuelekea Los Angeles. Watoto hao hawakuwa wake peke yake, bali baba yao alikuwa Mike ambaye naye alikuwa bilionea mkubwa.


Wakapanga mikakati ni kwa namna gani wangewatunza watoto hao, hivyo siku hiyohiyo Mike kumsindikiza kuelekea Los Angeles kwa ndege yake binafsi. Huku nyuma, hata vijana ambao walifanya utekaji wakaachiwa huru kwani kesi yenyewe ikagundulika kwamba watoto hawakutekwa bali walichukuliwa na baba yao, mjadala ukaishia hapo.


Wakafika mpaka Los Angeles ambapo wakapanga apartment na kuishi huko. Kwa kuwa Mike aliwapenda sana watoto wake, akaamua kuwanunulia nyuma ya kifahari, kuwawekea kila kitu na kumtaka Katty aishia nao huko.


Kila siku Katty akawa mtu wa kupokea meseji na kupigiwa simu na Dylan na kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea, hakujibu meseji hizo kwani mwanaume huyo alimuumiza moyo wake kupita kawaida.


Siku zikaendelea, watoto wakakua, Dylan akaendelea na maisha yake yenye uchungu, ya kulia kila siku. Hakuwa na furaha hata siku moja, aliwakumbuka Patrick na Patricia lakini hakuwa na jinsi, hawakuwa watoto wake.


Hayo mambo yalimalizwa kimyakimya, hata maofisa wa FBI walipewa fedha nyingi kutunza siri, hakikutakiwa kujulikana kitu chochote kile. Kutokana na kuwa na msongo wa mawazo, afya ya Dylan ikaanza kuzorota, akaanza kukonda, akawa hali na baada ya kwenda hospitali kupimwa, akagundulika kuwa na shinikizo la damu ambalo lilimfanya kudhoofika kila siku mpaka kufikia hatua ya kupelekwa hospitali.


Afya yake haikubadilika, bado aliendelea kuumia kila siku, akakosa amani, furaha ikapotea, fedha hazikumsaidia, hazikuweza kuinunua afya na kurudi kama zamani.


Kuumwa kwake ukawa gumzo duniani kote, kila kona watu walimzungumzia yeye, kila mmoja alisema lake, kwa jinsi alivyokuwa amedhoofika kitandani pale kila mmoja aliamini kwamba Bwana Dylan asingeweza kupona, angekufa palepale kitandani.


Maneno ya watu hao yakawa kama sumu kwani tangu watu wawe na hofu namna hiyo na kutamka maneno mabaya, Dylan hakuchukua muda mrefu, akafariki kitandani hapo.


Ilikuwa ni huzuni mno, watu walisikitika kwani alikuwa mtu mwema, aliyewasaidia watu wengi ila mwisho wa siku, shinikizo la damu likamuua kitandani hapo.


Katika mazishi yake, Katty hakuacha kwenda, alikwenda ila hakwenda na watoto kwa kuwa huyo hakuwa baba yao, ndugu za Dylan walikuwa wakimwangalia kwa jicho baya lakini hakutaka kujali, alichojua alikwenda hapo kwa ajili ya kuonyesha ushirikiano na kwa kuwa alimpenda Dylan, hakukuwa na kingine.


Baada ya siku mbili, Dylan akazikwa katika makaburi ya Victoria Cementary yaliyokuwa New Orleans ambapo ndipo alipokuwa amezaliwa, sehemu ambayo wazazi wake walikuwa wakiishi hata kabla ya kupata utajiri.


Baada ya mazishi hayo, Katty akarudi zake Los Angeles ambapo aliendelea kuwalea watoto wake. Hakuhitaji urithi, hakuhitaji kitu chochote kutoka katika familia ya Bwana James, aliwaacha na utajiri wao, yeye aliendelea kufanya vitu vyake huku Mike akimtunza na kumfungulia biashara mbalimbali za kufanya ambazo zilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha.


MWISHO.